USAJILI mzito ambao unaendelea kufanywa na Uongozi wa klabu ya Yanga umezidi kuwapa jeuri, ambapo sasa wameweka wazi kuwa wanataka kuweka rekodi ya kufanya vizuri zaidi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.
Yanga mpaka sasa wamekamilisha na kuwatangaza wachezaji watano ambao ni Wakongomani, Heritier Makambo na Fiston Mayele, mshambuliaji mzawa Yusuph Athuman, kiungo Mganda, Khalid Aucho na mlinda mlango wa Mali, Djigui Diara huku ikiwa katika harakati za kuyatangaza majembe mapya Shaban Djuma, Yannick Bangala Litombo.
Yanga msimu ujao itakuwa miongoni mwa timu nne zitakazoiwakilisha Tanzania Bara katika michuano ya Kimataifa ambapo watashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akizungumzia mipango yao kuelekea michuano ya Kimataifa, Mkurugenzi wa mashindano wa Yanga, Thabit Kandoro amesema: “Kikosi chetu kinaendelea kufanya usajili mkubwa kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao, tayari tumewatambulisha rasmi baadhi ya wachezaji, na kuna majembe zaidi yanakuja.
“Malengo yetu ni kufanya vizuri msimu ujao kwenye michuano mbalimbali tutakayoshiriki, lakini malengo yetu makubwa zaidi ni michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo tunataka kuandika rekodi ambayo haijawahi kufikiwa na timu za Tanzania.”