LICHA ya klabu kubwa nchini Simba, Yanga na Azam FC kupokea kwa mikono miwili ruksa ya kusajili wachezaji 12 wa kigeni kuanzia msimu huu, serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT), imesema bado haijatoa tamko lolote kuhusu ongezeko hilo.
Kwa mujibu wa kanuni za msimu uliopita, kila klabu ya Ligi Kuu iliruhusiwa kusajili wachezaji 10 wakigeni huku ikiruhusiwa kuwachezesha wote katika mchezo mmoja, lakini msimu huu Shirikisho la Soka nchini (TFF) kupitia Bodi yake ya Ligi (TPLB), imefanyia marekebisho kanuni zake ambapo sasa kila klabu inaweza kusajili ‘mapro’ 10 wakigeni lakini ikiruhusiwa kuwachezesha nane tu katika mchezo mmoja.
Akizungumza jana, Ofisa Uhusiano wa BMT, Najaha Bakari, alisema walipokea barua ya maombi ya ongezeko hilo kutoka TFF, lakini bado serikali haijatoa majibu yoyote kukubali au kukataa.
Alisema awali walipokea maombi kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusu kuongezeka kwa idadi ya wachezaji wakigeni na wakiwa kwenye mchakato huo wa kufanyia kazi mapendekezo hayo, walishangazwa kuona TFF tayari imeshatoa maamuzi kabla ya majibu kutoka.
“Ni kweli TFF walileta barua ya maombi kwetu juu ya kuhitaji kuongeza idadi ya wachezaji wa kigeni kuwa 12, lakini kabla ya serikali kutoa tamko kuhusu hilo, wameanza mchakato huo na timu tayari zimesajili nyota hao ambao nane wataruhusiwa kucheza katika mechi mmoja wa ligi,” alisema Najaha.
Alisema serikali itatoa tamko rasmi kuhusu idadi hiyo ya wachezaji 12 baada ya kumalizika kwa mchakato ambao walifanya kupitia wadau mbalimbali kupata maoni yao kuhusu usajili wa idadi ya nyota hao kwa klabu za Ligi Kuu Tanzania Bara.