Home Makala MUDA WA KUANZA KUPATA HASIRA UPO KWENYE KONA KWA SASA

MUDA WA KUANZA KUPATA HASIRA UPO KWENYE KONA KWA SASA


 HESABU za usajili ndani ya ardhi ya Bongo zinatarajiwa kufungwa Agosti 31 baada ya kuwa na muda wa mwezi hivi katika purukushani za kusaka wachezaji wapya.

Kila kitu kwa sasa kwa asilimia kubwa kipo wazi kwani zipo timu ambazo zilifunga kabisa masuala ya usajili ikiwa ni pamoja na Azam FC, Biashara United hawa walimaliza shughuli mapema kabisa.

Wale ambao bado wapo sokoni ni muda wao wa kufunga hesabu kwani hakuna tena muda wa kuongeza. Taarifa rasmi kutoka Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) iliweza kubainisha suala hilo.

Jambo la msingi kwa sasa kwa zile ambazo hazijakamilisha zipambane kufikia malengo kwani bila kufanya hivyo mambo yatakwenda mrama.

Muda ule ambao unasubiriwa kwa shauku kubwa na wadau ni ligi kuanza. Huo muda kwa sasa upo kwenye kona unakaribia kutua na mambo yataanza kuwa hewani kama kawaida.Wakati ule wa hasira kwa timu ambayo itakwama kufikia malengo na wachezaji ambao mambo yatakuwa magumu kwao.

Kama vile ambavyo ulianza usajili kwa kasi na ghafla kwa sasa ni siku tu inahesabiwa kisha mambo yanakuwa mengine ndivyo ambavyo itakuwa hivyo hata muda ue wa lawama utakavyofika.

Ikishachezwa mechi ya Ngao ya Jamii kati ya Simba na Yanga mambo yanakuwa yapo karibu. Ni muda wa kujua nani alipanda kwa wakati sahihi na nani alikurupuka kupanda.

Haina tabu kubwa sana kwenye kutambua nani aliweza kwenda na wakati kwa kuwa mavuno yake yanaonekana na ipo wazi kabisa.

Mavuno ya kile ambacho kimepandwa wakati wa usajili pamoja na maandalizi ya ligi kwa ujumla huwa yanapatikana ndani ya dakika 90 za ushindani.

Hapo kila mmoja anakwenda kujua maana halisi ya rangi ambayo ilikuwa imepambwa kama ni nyekundu ama nyeupe wakati ule wa usajili na maandalizi ya ligi kwa ujumla.

Ni muda wa kwenda kuwaona wale makipa ambao tumeambiwa kwamba wanadaka mpaka mishale wakiwa langoni.

Kazi ipo kwa kuwa kila mmoja anatamba kuwa na timu imara na bora. Basi kipimo cha ubora kinakuja na uthibitisho utapatikana.

SOMA NA HII  WAKATI AKIJIANDAA NA SIMBA..BABA WA DICKON JOB AFICHUA MWANAYE ALIVYOLOGWA YANGA...

Ipo wazi kabisa kwamba zipo timu ambazo zinakwenda kuanza kwa anguko katika mzunguko wa kwanza kwa sababu maandalizi yao yamekuwa ni ya kawaida.

Kwa hawa lazima wajipange mapema kwa kuanza kuangalia gia ambayo wataanza nayo na kuibadili mapema kabla ya mzunguko wa pili.

Mzunguko huu wa kwanza mara nyingi imekuwa kawaida timu kuuchukulia kama ni wa majaribio jambo ambalo huwa linakuja kuwagharimu baadaye hasa kwenye mzunguko wa pili.

Kwa timu ambayo imeweka malengo makubwa lazima hesabu zianze kufanya kazi wakati huu ili hata ule muda wa jioni utakapofika kila mmoja awe ana kitu cha kuanzia.

Sio inafika jioni katika mzunguko wa pili hapo watu wanaanza kutafuta pakutokea, itafahamika tu kama ilikuwa ni nyekundu ama nyeupe.