MUASISI wa Simba Day, Hassan Dalali ametoa hamasa kwa mashabiki wa timu hiyo, kujitokeza kwa wingi Septemba 19, ili kudhihirisha wao ndio waanzilishi wa tamasha hilo na Yanga wakaiga.
Dalali aliyeanzisha tamasha hilo mwaka 2009 na walicheza mechi dhidi ya Villa ya Uganda, alisema ameona kila mwaka kuna hatua kubwa inayopigwa kuhusu tamasha hilo, hivyo anaamini mwaka huu litafunika zaidi.
“Tayari viongozi wametangaza tarehe ya tamasha hilo, hivyo niwaombe mashabiki wa Simba ndani na nje ya Tanzania, waje kwa wingi kuhakikisha wanaonyesha wao ndio waanzilishi wa tamasha hilo na wengine wameiga,” alisema Dalali na aliongeza;
“Sina shaka na viongozi wa Simba kuja na mambo makubwa zaidi, hivyo tunatakiwa kuungana kwa pamoja kuhakikisha kinafanyika kitu cha kuacha historia yenye mafunzo.”
Dalali alisema tamasha la kwanza alipata Sh70 milioni na milioni 20 zilitumika kununulia Uwanja wa Bunju (Mo Simba Arena).
Septemba 19, utakuwa mwaka 12 kwa timu hiyo kufanya tamasha hilo, hivyo Dalali alisisitiza wafanye vitu vitakavyoendana na ukomavu wao.
Mbali na Dalali, wadau mbalimbali waliotoa mitazamo yao juu ya tamasha hilo.
Aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ alisema Dalali anastahili kujengewa hadi nyumba, kutokana na wazo lake la Simba Day linalozalisha pesa nyingi na limekuwa mfano wa kuigwa ndani na nje huku likiwashawishi hadi watani zao Yanga kuanzisha na wao kuliita Wiki ya Mwananchi.
“Ingekuwa mimi ningemjengea nyumba. Ningemfanyia makubwa yatakayompa faraja kwa kazi aliyoianzisha na sasa inailipa klabu pesa za maana. Anastahili kupewa tuzo siku hiyo.”
Naye Ulimboka Mwakingwe alisema wakati Simba Day inaanzishwa alikuwa anaichezea timu hiyo na walicheza dhidi ya Villa ya Uganda iliyoalikwa na kutoa ushauri kwa viongozi wa klabu hiyo kumwangalia kwa jicho kubwa Dalali.
“Ni kiongozi aliyefanya makubwa. Siku hiyo anastahili heshima na kama hajawahi kupewa tuzo, viongozi waliopo walifikirie hilo kwani ni jambo muhimu sana na afanyiwe jambo litakaloienzi kazi yake,” alisema.
Kuhusu tamasha la kilele cha Wiki ya Mwananchi linalofanywa na Yanga, Makingwe alisema kwa upande wa watani zao walifanya jambo kubwa na anaamini hilo litawapa chachu Simba kufanya kubwa zaidi.
Naye, Emmanuel Gabriel alimsifia Dalali kwa kununua uwanja na kuhamasisha matawi kuwa na mchango kwenye timu.
“Lazima tumpe sifa zake akiwa hai, Dalali alifanya matawi yawe na nguvu, alianzisha Simba Day kwa ajili ya kununua uwanja, hivyo viongozi waliopo lazima wajue mchango wa huyo mzee na wampe heshima yake siku hiyo,” alisema.
Simba wamesisitiza tamasha la mwaka huu litakuwa la aina yake na kuna mambo wameyapangilia yatakayokuwa sapraizi kwa mashabiki na wanachama.