Home news PAMOJA NA KUFUNGA GOLI JUZI..MAKAMBO BADO ‘ANAWENGE ‘..AWATAJA SIMBA SC

PAMOJA NA KUFUNGA GOLI JUZI..MAKAMBO BADO ‘ANAWENGE ‘..AWATAJA SIMBA SC


MSHAMBULIAJI mpya wa Yanga, Heritier Makambo amewasisitiza mashabiki kutulia kwani ndio kwanza wanaanza kazi. Amesema katika msimu ujao kwenye Ligi Kuu Bara ambao utaanza Septemba 29, malengo yake ni kufunga zaidi ya mabao ambayo alifunga mara ya mwisho alipocheza soka hapa nchini.

Ameenda mbali zaidi kwa kuwachokoza watani wao wa jadi Simba kuwa waje tu sababu Yanga haina hofu ya kukutana nao kwani kikosi inarudi kambini kujiweka sawa tayari kwa kazi.

Makambo alicheza katika kikosi cha Yanga msimu 2018-19, ambao alimaliza na mabao 17, matano nyuma ya mfungaji bora, Meddie Kagere (Simba), aliyemaliza na 23, kisha baada ya hapo alitimkia Horoya ya Guinea.

Straika huyo raia wa DR Congo alisema muda utaongea kutokana na kikosi chao kilivyo bora msimu huu na matokeo ya juzi dhidi ya Zanaco wala yasiwape huzuni mashabiki wao kwani walipata changamoto ya maandalizi ya msimu mpya.

“Hatukuwa na maandalizi mazuri ya msimu (Pre-season), kutokana na sababu mbalimbali lakini wachezaji tuliokuwepo tukikaa kwa pamoja ndani ya muda mfupi naiona Yanga iliyo bora na imara msimu ujao.

“Nataka kupambana na kufunga mabao ili kufikia na hata kuipitai rekodi yangu niliyofunga mara ya mwisho hapa Tanzania, naamini hilo linawezekana,” alisema Makambo ambaye alifunga bao la pekee katika mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Zanaco iliyomaliza kwa Yanga kulala kwa mabao 2-1.

Makambo alisema kikosi cha msimu huu ni tofauti na wakati anaondoka kwani wadhamini wao GSM, wamesajili wachezaji wenye kiwango bora na uwezo wa kucheza soka.

“Baada ya hapa tutaendelea na mazoezi ili kutafuta muunganiko wa timu kwani wachezaji wengi ni wageni bado hatujazoeana na tukishakuwa fiti basi mashabiki wetu wategemee furaha.

“Najua mechi ya ufunguzi wa ligi tutacheza na Simba, hivyo wala siwahofii, waje tu na mashabiki wafike kwa wingi siku hiyo, tunawaahidi mambo mazuri,” alisema.

Katika hatua nyingine, Abeid Mziba mpachika mabao nyota wa zamani wa Yanga, alisema Makambo yuko kwenye kiwango bora na hakuna shaka atawasaidia Yanga.

SOMA NA HII  KWA KAULI HII YA KITASA KIPYA CHA JANGWANI....MASHABIKI YANGA MSIPOANGALI MTAUMWA KISUKARI...

“Amecheza vizuri sana na bado yuko kwenye kiwango bora, kifupi ameanza vizuri, si peke yake bali wachezaji wengi wapya na hata wazawa wamecheza kwa kiwango bora, wanahitaji maboresho kidogo tu ili kupata muunganiko bora ambao utaifanya timu hiyo kuwa tishio,” alisema Mziba.

Kwa upande wa staa wa zamani wa Yanga, Ally Mayay alisema: “Makambo kaanza vizuri, bado yuko kwenye kiwango kile kile kama alivyoondoka Yanga hivyo kama akiendelea hivyo ataisaidia timu.”

Alisema Yanga walipwaya eneo la beki wa kati kwani walikosa mawasiliano kwa kiasi kikubwa na ndio wameigharimu timu, pia kukosa utimamu wa mwili imechangia wao kushindwa kuonyesha ushindani na hasa kipindi cha pili.

“Mabeki wa kati walikuwa wanatoka wote kwa pamoja, pia Shaban Djuma sio beki halisi ni mtu ambaye anapenda kushambulia anatoka sana eneo lake na anachelewa kurudi, kama wapinzani wao wangelisoma hilo basi tungekuwa tunazungumza mengine. Anaonekana ni mzuri zaidi akicheza kama winga.

“Makambo amerudi wakati sahihi na amekuja kuziba pengo ambalo Yanga limewasumbua kwa muda mrefu akisaidiana na Jesus Moloko winga ambaye alionyesha kupandisha mashambulizi mara kwa mara na kupiga krosi nyingi ambazo hazikuzaa matunda lakini muunganiko wao unaweza kuwa na tija kwa Yanga,” alisema.