UONGOZI wa Simba umeweka wazi kuwa mauzo ya jezi zao za msimu ujao wa 2021/22, yameandika historia mpya katika biashara ya jezi nchini ambapo mpaka sasa tayari zaidi ya jezi 42,000 zimeshauzwa.
Simba Ijumaa iliyopita walitangaza rasmi kuanza kuuzwa kwa jezi mpya za klabu hiyo zinazopatikana kwenye maduka ya mzabuni, na mbunifu wa jezi hizo kampuni ya Vunjabei, huku gharama yake ikiwa ni Shilingi 35,000 kwa jezi za wakubwa na 25,000 kwa jezi za watoto, ambapo mpaka sasa inaelezwa tayari zaidi ya Shilingi bilioni 1.4 zimekusanywa kupitia mauzo ya jezi hizo.
Tangu kuanza kuuzwa kwake, jezi hizo zimekuwa gumzo kubwa kwenye mitandao ya kijamii, huku mashabiki wengi wa klabu hiyo wakijitokeza katika maduka ya Viunjabei na mawakala wake kwa ajili ya kuzinunua.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Kaimu Ofisa habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema: “Tumeweka historia mpya ya mauzo ya jezi kwa upande wa klabu hapa nchini kupitia jezi zetu za Simba kwa msimu ujao wa 2021/22, ambapo mpaka sasa zaidi ya jezi 42,000 zimeshauzwa.
“Bado tunaendelea kufanya mapitio mapya ya takwimu hizi kwa kuwa, mashabiki wa Simba wanazidi kuzinunua kwa kasi tangu kuzinduliwa rasmi mtandaoni siku ya Ijumaa, ni wazi sasa hata Vunjabei mwenyewe anajivunia kuwekeza kwenye klabu kubwa kama Simba.”