TAYARI Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Mohamed Dewji ‘Mo’, ameitisha kikao cha haraka na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Didier Gomes Da Rosa kwa ajili ya kuhakikisha wanapata mbinu sahihi za kuimaliza Yanga kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii.
Simba inatarajiwa kuwa mwenyeji katika mchezo huo dhidi ya Watani wao wa Jadi, Yanga Septemba 25, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.
Katika mchezo huo, Simba inaingia na kumbukumbu ya kupoteza bao 1-0, dhidi ya TP Mazembe katika mechi iliyopita ya kilele cha maadhimisho ya Simba Day, wakati Yanga nayo inaingia ikiwa na hasira ya kung’olewa kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mbele ya Rivers United ya Nigeria kwa jumla ya mabao 2-0.
Chanzo chetu kutoka ndani ya Simba, kimeliambia Championi Jumatano kwamba, tangu Simba iingie katika kambi yake ya nchini Morocco kisha Karatu jijini Arusha, Mo, hakuwepo nchini, lakini alirejea siku ya Simba Day na baada ya shughuli hiyo aliwaita Gomes na Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Barbara Gonzalez kufanya kikao cha dharura.
“Tayari maandalizi kuelekea katika mchezo wetu na Yanga, kimsingi naweza kusema yameshaanza kwani baada ya tamasha letu la Simba Day timu ilipewa mapumziko mafupi ya siku moja, huku Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mo Dewji akiitisha kikao cha fasta na kocha Gomes na CEO Barbara.
“Kikao ambacho kilihusisha watu watatu tu kikiwa na lengo la kujadiliana juu ya mchezo huo lakini na mwelekeo mzima katika mashindano yote yajayo.
“Tayari timu ipo kambini na imeshaanza programu zote za mazoezi hivyo mipango yote iliyojadiliwa katika kikao hicho tayari kocha ameshaanza kuifanyia kazi hivyo hatuna shaka yoyote ya kuibuka na ushindi kuelekea mchezo huo muhimu kwetu.”
Mchezo huo unasubiriwa kwa shauku kubwa na mashabiki wa nje na ndani ya Tanzania ili kuweza kuona nani ataibuka kuwa mbabe.