Home Makala NDEMLA UMELIKUNG’UTA VUMBI, SASA NI WAKATI WAKO KUONYESHA UWEZO

NDEMLA UMELIKUNG’UTA VUMBI, SASA NI WAKATI WAKO KUONYESHA UWEZO


 HATIMAYE yale niliyoyapigia kelele kwa muda mwingi sana nimeyaona yakitimia na sasa unaweza ukawa ni wakati wa utekelezaji na mafunzo mengine ya maisha.

 

Kawaida katika maisha kila jambo linakuwa na mafunzo yake kutokana na hali ilivyo. Jambo linazungumziwa, baadaye linatokea na baada ya hapo kuna mwendelezo.

 

Said Khamis Ndemla amekubali kujiunga na Mtibwa Sugar ya Turiani mkoani Morogoro. Jambo ambalo bila shaka wapenda mpira wengi hawakulitarajia.

 

Limeonekana ni kama jambo la kushitukiza hivi kwa mambo matatu. Kwanza halikuwa na gumzo kwenda kutokea kwake, pili Ndemla na Simba wamekuwa kimya kuhusiana na hilo na tatu hakukuwa na upande wowote ulionyesha kutoridhishwa na kufikiwa kwa uamuzi wa jambo hilo.

 

Hayo tuyaache, kidogo turejee nyuma. Kama unakumbuka leo ni zaidi ya msimu wa sita Ndemla anaendelea kuwa katika kikosi cha Simba na ameendelea kuwa mchezaji asiye tegemeo.

 

Kila Simba inapobadili kikosi, basi mara nyingi yeye ameendelea kuwa mchezaji anayetokea benchi na wengine wengi wametua Simba, wakafanya yao na kupata mafanikio na yeye akaendelea kubaki benchi akiwa mchezaji wa akiba.

 

Mara kadhaa kila alipopata nafasi ya kucheza, Ndemla ameonyesha uwezo mkubwa katika kikosi cha Simba na akafanya vizuri. Lakini bado kutokana na Simba inavyozidi kukua kwa kasi kubwa, imeonekana bado Ndemla hana nafasi ya kuwa mchezaji wa kwanza na tegemeo katika kikosi cha Simba.

 

Hata wale waliotokea nje ya Simba na kujiunga nayo, mfano wa Mzamiru Yassin na wengine, angalau wanaweza kuwa na nafasi kubwa ya kucheza au kuanza kuliko Ndemla ambaye bila shaka hakuna ambaye anaweza kuwa na hofu ya uwezo wake.

 

Angalia wachezaji kariba ya Feisal Toto wa Yanga, ni aina inayofanana na wachezaji kama Ndemla. Lakini kipaji chake kiliendelea kudumaa na kupotea na mavumbi ya benchi na ndio maana nilipiga kelele muda mrefu sana nikieleza ambavyo niliona si sahihi kwa Ndemla kuendelea kuchakaa na mavumbi ya benchi bila ya sababu za msingi.

 

Kama unakumbuka zaidi ya miaka mitano, Ndemla aliibuka shujaa akiingia uwanjani baada ya mapumziko na kuisaidia Simba kurejea mabao matatu baada ya kuwa chini kwa mabao 3-0 dhidi ya Yanga, mechi ambayo wengi walitabiri Simba inakwenda kufungwa mabao saba katika kipindi cha pili!

SOMA NA HII  OSCAR OSCAR : TATIZO SIO CHAMA NA LUIS KUONDOKA SIMBA..TATIZO NI....

 

Jiulize, shujaa akiwa kinda, vipi ashindwe kuwa tegemeo katika kipindi ambacho ana ubora zaidi kiuchezaji. Uwezo wa kuchezesha, uwezo wa kukaba, ubora wa pasi na hata ubora wa upigaji mashuti kuliko ikiwezekana wachezaji wote wa Ligi Kuu Bara kwa kipindi hiki. Maana yake, ilikuwa ni lazima Ndemla awe nje ya Simba ili kupata nafasi ya kujiuliza na kuna nafasi ya kurejea akiwa na nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza. Maana hili linabaki mikononi mwake.

 

Leo Ndemla ameamka na kukubali kukung’uta vumbi lililokuwa limemzunguka kutoka mabenchi ya makocha zaidi ya wanne wa kigeni na baadhi wazalendo na kuamua kurudi kwenda kuanza upya. Huu ni uamuzi ninaamini kamwe hawezi kuujutia kama ataamua kuwa makini na kuifanya kazi yake kwa kiwango cha weledi wa juu kabisa.

 

Ndemla ana uwezo mkubwa sana, ninaamini hata makocha wengi ambao hawa kumuamini sana huenda walikuwa na ulevi wa kuamini wageni zaidi lakini Ndemla ana uwezo wa mambo mengi ambayo wageni wengi hawakuwa nayo hata ndani ya kikosi cha Simba.

 

Katika mpira huu ni mfumo, wakati mwingine unalazimika kurejea chini ili kupata nafasi ya kuanza upya kwa wakati mwingine tena na inawezekana ukawa una nafasi nzuri ya kufikia malengo yako ambayo yalikuwa yanakutatiza wakati ukionekana ukiwa umekaribia kabisa.

 

Binafsi ninaona Ndemla amechelewa kwa kuwa alipaswa kuondoka Simba angalau misimu miwili iliyopita. Lakini inawezekana ulikuwa ni uamuzi mgumu kuufanya na huenda miruzi mingi kutoka kwa watu wengi ilikuwa inampoteza.

 

Nakumbuka kila nilipoandika makala nikishauri anapaswa kuondoka, wako walinishambulia kwa maneno mengi kwamba nataka kumuondoa Simba na kadhalika. Leo uhalisia ndio huu na Ndemla ametulia na kuona ukweli wa mambo na alichofanya ni sahihi kabisa.

 

Amekwenda timu sahihi kwa maana ya matunzo ya wachezaji, timu ambayo licha ya kuwa imekuwa katika wakati mgumu kwa vipindi vya misimu kama minne hivi, lakini inaonekana imeamua kubadilika katika usajili lakini ndipo wachezaji wengi ambao huonekana wameisha au hawafai, wamekuwa wakipewa dawa ya kuinuka na kuwa tegemeo kwa klabu na hata timu zetu za taifa.


Imeandikwa na Saleh Ally