Home news SIMBA, YANGA WAIBIANA MBINU, KAZIKAZI KOTE MPAKA KIELEWEKE

SIMBA, YANGA WAIBIANA MBINU, KAZIKAZI KOTE MPAKA KIELEWEKE


 KATIKA kuhakikisha wanarejea wakiwa imara kwa ajili ya ushindani, Kocha Mkuu wa Simba, Mfaransa, Didier Gomes na Kocha wa Yanga, Mtunisia, Nasreddine Nabi, ni kama wameanza kuigana kwenye mbinu za kuzifanya timu zao kuwa imara zaidi.

Hiyo ni baada ya kila upande kuanzisha program ya mazoezi mara mbili kwa siku tofauti na hapo awali. Awali timu hizo wakati zikiwa katika maandalizi ya michezo ya Ligi Kuu Bara, zilikuwa zikifanya program moja pekee za mazoezi asubuhi, huku jioni wakipewa mapumziko.

Akizungumza na Spoti Xtra, Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema tangu waliporudi kambini Jumatatu wiki hii, Nabi anawafanyisha mazoezi wachezaji wake mara mbili kwa siku moja.

Saleh alisema lengo ni kutengeneza muunganiko wa timu na fitinesi kipindi hiki ligi imesimama kuhakikisha vijana wake wanakuwa fiti na tayari kwa mapambano.


“Kocha amewaongezea program za mazoezi wachezaji, hii ni baada ya kuona upungufu katika michezo miwili ya ligi ambayo wamecheza.

“Hivyo wanafanya asubuhi na jioni kwa wachezaji wote ili kuhakikisha wanakuwa fiti na tayari kupambana ikiwemo kuiboresha safu yake ya ushambuliaji ambayo amekuwa akiilalamikia,” alisema Saleh.

Wakati mambo ya Yanga yakiwa hivyo, kwa upande wa Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, alisema: “Tangu tuliporejea mazoezini Jumatatu, timu imekuwa ikifanya mazoezi mara mbili kwa siku Uwanja wa Boko Veteran.


“Licha ya uchache wa wachezaji wetu mazoezini lakini program hizo zinaendelea kufanyika kwa ufasaha. Wachezaji wetu 16 wapo katika majukumu ya timu zao za taifa lakini mambo mengine yanaendelea.”

SOMA NA HII  HII HAPA NJIA YA MAYELE KUIBUKA MFUNGAJI BORA AFRIKA...MECHI MBILI TU ANABEBA KIATU CHA DHAHABU....