SHOMARI Kapombe beki wa Klabu ya Simba ambaye ni chaguo la kwanza mbele ya Kocha Mkuu, Didier Gomes amepewa nyota za kutosha na kocha huyo kwa kitendo chake cha kuwa kiongozi mzuri pamoja na akili za kutosha uwanjani.
Kwenye mechi ya kwanza ya ligi ambayo alicheza dhidi ya Biashara United alipata maumivu na alitumia dakika 49.
Kwenye mchezo huo alikuwa amevaa kitambaa cha unahodha alikosekana kwenye mchezo wa pili dhidi ya Dodoma Jiji uliochezwa Uwanja wa Jamhuri,Dodoma.
Gomes amesema kuwa anafurahishwa na uwezo wa Kapombe akiwa uwanjani ikiwa ni pamoja na namna ambavyo anaongoza hivyo matumaini yake ni kuona kwamba anarejea uwanjani kuendelea kuipambania timu.
“Kapombe ni mchezaji mzuri na anaonyesha hilo akiwa uwanjani kwa kuwa anatumia akili na nguvu pia, kwa namna ambavyo anakuwa na uwezo wa kuongoza hii inamaanisha kwamba ni mchezaji muhimu na wa nyota ya juu.
“Muda huu bado hajawa fiti lakini tuna amini kwamba atarudi na kuendelea na majukumu yake baada ya muda si mrefu hivyo tunaamini kwamba ataendelea kutimiza majukumu bila matatizo,” amesema Gomes.
Jana, Oktoba 11 kwenye mazoezi Kapombe alianza kufanya mazoezi na wachezaji wenzake ambao wanakazi ya kucheza na Jwaneng Galaxy ya Botswana unaotarajiwa kuchezwa Oktoba 17.