MASTAA wawili wa Yanga, Fiston Mayele na Jesus Moloko yamewakuta mazito uwanjani. Wameweka wazi katika mechi mbili za ligi walizocheza wamekumbana na mambo ambayo hawakuyatarajia lakini inaonekana ni kitu cha kawaida.
Mastaa hao wamecheza dakika 180 za Ligi na 90 dhidi ya Simba kwenye Ngao ya Jamii.
Mayele aliyehusika na mabao mawili katika mechi hizo tatu, akihojiwa na Gazeti la Mwanaspoti ameweka wazi amekuwa akiumizwa sana tena makusudi na kama angekuwa mlaini angeshakaa nje kwa majeruhi.
Pia amesema ameshuhudia matusi makali kutoka wachezaji wa timu pinzani, lengo likiwa ni kumtoa mchezoni, hata hivyo wameshindwa kwani anasikia vizuri lugha ya Kiswahili tofauti na Moloko.
Mayele alisema amepigwa sana viatu na katika miguu yake amechanwa mara tatu na kuachiwa vidonda na mara zote amekuwa akilalamikia waamuzi lakini haoni wakifanya uamuzi ndani ya uwanja.
Licha ya wachezaji hao kumfuata na kumpa mkono wa pole wakiashiria kutimiza mchezo wa kiungwana ‘Fairplay’ lakini anafahamu hayo wamekuwa wakifanya kwa kukusudia ili kumpunguza makali. “Wameniumiza sana katika mechi hizi tatu, ilinihitajika kuwa na roho ngumu sana vinginevyo unaweza kupata matatizo,” alisema na kuongeza, “Angalia hivi vidonda vyote nimevipata katika mechi hizi tatu tu,” alisema Mayele huku akionyesha sehemu alizoumia kwa masikitiko ingawa alikiri kwa nafasi yake ni lazima kukumbana na changamoto kama hizo, lakini siyo kwa kiwango alichokumbana nacho kwenye mechi za mwanzo za ligi ya Tanzania.
Mbali na majeraha hayo, pia Mayele amefichua mabeki hao wamekuwa wakimtamkia matusi mengi wakati akiwa uwanjani. “Wanatukana sana najua beki kuna wakati anataka kukutoa katika utulivu wa akili akuonyeshe yeye ni mtu mgumu lakini sipendi sana matusi au lugha chafu kama hizi, ni jambo la ajabu sana,” amesema.
Kauli hiyo ya Mayele imeungwa mkono na winga wao, Jesus Moloko akisema;
“Kweli wanatumia lugha kali sana. Yapo matusi makubwa mimi sijui Kiswahili lakini nimejua haya matusi baada ya kuuliza wanavyosema lakini hakuna shida najua malengo yao, nitawakomesha,” alisema.
Hata hivyo, Mayele ambaye amesajiliwa na Yanga akitokea AS Vita alisema rapsha alizokumbana nazo kwenye mechi hizo zimemwonyesha uhalisia wa ligi ya Tanzania na amepata mbinu za kupambana zaidi kutupia langoni kwani anajua kiu ya mashabiki.
“Mtu akitumia nguvu na mimi natumia nguvu mimi sio mchezaji laini laini, akiniumiza sitarudisha wala akinitukana sitarudisha ila nitakachofanya ni kupambana niwafunge, hilo ndio litakuwa jibu langu zuri kwao, siwezi kukatishwa tamaa.”