KOCHA Mkuu wa Simba Mfaransa, Didier Gomes amesema kuwa kiungo wake mkabaji Jonas Mkude bado ana nafasi ya kucheza katika kikosi chake cha kwanza.
Kauli hiyo ameitoa ikiwa ni siku chache kabla ya timu hiyo kukwea pipa kwenda nchini Botswana kucheza mchezo wa hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy ambao Simba SC walishinda kwa goli mbili bila.
Mkude ameonekana kupoteza nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza tangu kiungo mpya mkabaji raia wa Mali Sadio Kanoute atue msimu huu.
Gomes alisema kuwa hakuna mchezaji yeyote mwenye nafasi ya kucheza katika kikosi chake cha kwanza.
Gomes alisema kikubwa anachokiangalia ni kiwango cha mchezaji mazoezini kila siku na ana mpanga baada ya kuonyesha kiwango chake na siyo kitu kingine.
Aliongeza kuwa kama Mkude akionyesha kiwango bora cha kumshawishi, basi atampa nafasi ya kucheza kwa kumuondoa kiungo mmoja mkabaji kati ya Kanoute au Taddeo Lwanga.
“Katika timu yangu hakuna mchezaji mwenye nafasi ya kudumu ya kucheza katika kikosi cha kwanza, wote wana uwezo sawa.
“Hivyo Mkude na wachezaji wengine wote waliokuwepo katika kikosi changu wana nafasi na walichotofautiana ni vitu vichache pekee vya kiufundi ambavyo ni siri.
“Nimshauri aongezee bidii ya kujituma mazoezini ili ajihakikishie nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza, kwani ili ipate nafasi ya kucheza ni lazima mchezaji anishawishi mazoezini,” alisema Gomes.