JIJI la Mbeya litasimama kwa muda pale mashabiki wa Simba na Yanga mkoani hapa watakapokutana uwanjani katika tamasha maalumu kuwania kitita cha Sh 1 milioni, huku pande zote zikitamba kufanya kweli.
Tamasha hilo lililoandaliwa na kampuni ya Ticon Sports Agent, linatarajia kufanyika Oktoba 30 katika viwanja vya Chuo cha Uhasibu kwa kushirikisha mashabiki wa timu hizo kongwe nchini.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Aman George alisema tamasha hilo linalenga kuwaweka pamoja na kuondoa dhana potofu ya Simba na Yanga kuwa ni mahasimu bali ni watani wa jadi.
Alisema katika tukio hilo kubwa litajumuisha michezo mbalimbali kama soka, kukimbiza kuku, kuvuta kamba, netiboli na rede kwa wanawake. โLengo ni kuondoa dhana ya Simba na Yanga kuitwa maadui, bali ni watani wa jadi, lakini kutafuta vipaji vya vijana ili kuwasaidia,โ alisema George.
Mwenyekiti wa Simba mkoani hapa, Abel Edson alisema maandalizi yanaendelea vizuri ya kusuka timu yao na kwamba Oktoba 23 wataingia kambini rasmi kujiweka sawa.
โWatani zetu wajiandae kisaikolojia, tunajua hawana timu ya kutufunga, tunaendelea kuweka sawa mipango kuhakikisha tunabeba zawadi kwenye michezo yote,โ alisema Edson.
Mwenyekiti wa Yanga mkoani hapa, Chuma Mahinya alisema wamejipanga kushusha kikosi katili uwanjani kuhakikisha wanawanyamazisha watani zao.