IMEFICHUKA kuwa, sababu kubwa ya kiungo mkabaji wa Simba, Jonas Mkude kushindwa kusafiri na timu hiyo kwenda nchini Botswana kwa ajili ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy, ni kitendo cha mchezaji huyo kukosa ripoti ya vipimo vya afya.
Wachezaji 24 wa Simba waliondoka jioni ya Ijumaa kwa ndege ya kukodi kuelekea Gaborone, Botswana kwa ajili ya mchezo huo wa hatua ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika uliopigwa juzi Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa wa Botswana na Simba kushinda 2-0.
Chanzo kutoka ndani ya Simba kimelitonya gazeti la Spoti Xtra kuwa, Mkude alishindwa kusafiri kutokana na kukosa ripoti ya vipimo vyake vya afya ambavyo ni miongoni mwa mahitaji ya lazima kwa wachezaji wote wanaoshiriki michuano hiyo mikubwa Afrika.
“Ishu nzima ilikuwa hivi, siku chache kabla ya safari ya kuelekea Botswana kwa ajili ya mchezo wetu dhidi ya Galaxy, wachezaji na viongozi wote tulienda kufanya vipimo kwenye moja ya hospitali kubwa hapa nchini iliyopo Dar es Salaam (jina tunalo), akiwemo Mkude lakini baada ya kufika hospitalini hapo, Mkude akatoweka katika mazingira ya kutatanisha, licha ya juhudi za kumtafuta lakini hakupatikana.
“Cha ajabu siku ya pili alikuja kwenye mazoezi kama kawaida na alipoulizwa kuhusiana na kilichotokea hospitalini akajibu angekwenda kupima lakini haikuwa hivyo mpaka siku tunaondoka, alipoleta pasi yake ya kusafiria akaambiwa hawezi kusafiri kwa kuwa hana ripoti ya afya,” kilisema chanzo hicho.
Gazeti la Spoti Xtra lilimtafuta Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu kuzungumzia hilo, ambapo alisema: “Suala la Mkude kutosafiri na timu ni benchi la ufundi ndilo linaweza kutoa maelezo mazuri.
“Hii ni kwa sababu wao ndiyo wanajua wachezaji gani wanawahitaji kuendana na wapinzani wetu, hivyo nadhani ni maamuzi ya benchi la ufundi kuendana na uhitaji wa mchezo.
”Hii si mara ya kwanza kwa Mkude kuripotiwa kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu katika kikosi hicho ambapo mwishoni mwa msimu uliopita, Simba walilazimika kumuondoa katika kwenye mipango yao kutokana na vitendo hivyo kabla ya kurudishwa tena kikosini msimu huu.