KUUMIA kwa straika wa Simba, Chris Mugalu atakayekaa nje miezi miwili, huenda ikawa fursa kwa Meddie Kagere kurejesha heshima yake ya kuwa muhimu kwenye kikosi cha kwanza cha kocha Didier Gomes huku wadau wakisema sasa ni uhakika kwamba atang’ara au ashindwe yeye.
Baada ya Mugalu kutua Simba, ilionekana nafasi ya Kagere kuwa finyu kwenye kikosi cha kwanza tofauti na misimu miwili nyuma ambayo alichukua kiatu cha dhahabu kwa mfululizo.
Kocha Gomes, alionekana kumwamini zaidi Mugalu ambaye msimu ulioisha alimaliza na mabao 15, wakati Kagere akimaliza na mabao 14, licha ya kwamba hakuwa muhimu kwenye kikosi cha kwanza.
Gomes alikiri wazi kwamba Mugalu anapaswa kukaa nje ndani ya muda huo, kutokana na kusumbuliwa nyama za paja.
“Mugalu atakaa nje kwa miezi miwili ili kurejea kwenye afya njema, lakini kuondoka kwake hakumaanishi kwamba haitawezekana kupata matokeo, tuna kikosi kipana,” alisema Gomes.
Staa wa zamani wa Simba, Emmanuel Gabriel alisema bado anauamini uwezo wa Kagere kwamba atafanya maajabu msimu huu pia anamuombea Mugalu kupona haraka. “Natamani kuwaona wachezaji wote wa Simba kuwa na afya, ila pia ni fursa kwa Kagere kujituma na kurejea kwenye makali yake ya kucheka na nyavu kama ilivyokuwa msimu wa 2018/2019 mabao 23 na msimu wa 2019/20 alimaliza na mabao 22,” alisema Gabi Goal.