NI makosa makubwa kumuona Simba amelowa na ukadhani kuwa ni paka. Kocha aliyeachana na Wekundu wa Msimbazi, Didier Gomes amewaambia Yanga kuwa ubingwa msimu huu pia ni wa Simba.
Katika mahojiano maalum na Gazeti la Mwanaspoti, Gomes amesema licha ya mwanzo usioridhisha wa msimu uliochangia kuondoka kwake Msimbazi, Simba bado ina timu bora ya kubeba taji la tano mfululizo la Ligi Kuu Bara msimu huu na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho, ambako wameangukia baada ya kutolewa na kwenye Ligi ya Mabingwa.
KIKAO CHA MOTO
Gomes anakiri alikuwa katika kikao kizito na mabosi wa Simba na yeye ndio akaamua aachie majukumu yake kwa ajili ya heshima ya timu hiyo na yeye kuangalia mambo mengine ya kufanya.
Kocha huyo anasema kikao hicho kilikuwa kizuri kwa manufaa ya pande mbili na ndipo yeye akaona ni sahihi kukaa pembeni kwa sababu pia amefeli kuiingiza timu kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa, kinyume cha mkataba wake.
“Kikao kilikuwa kizuri na nadhani nimechukua uamuzi sahihi, kocha lazima ubebe makosa yote kwa sababu mimi ndio kiongozi katika benchi la ufundi, siwezi kuzungumza sana,” anasema Gomes.
ISHU YA VYETI
Gomes anakiri kutokuwa na leseni A ya Caf huku yeye akimiliki leseni A ya Uefa, lakini amejikuta akishindwa kukaa katika benchi wakati Simba wakiwa wanacheza mashindano ya Caf.
Kocha huyo anasema kwa kukosa vyeti hivyo, njia pekee ambayo ingemwezesha kukaa kwenye benchi katika michuano ya Caf ni kama tu Simba ingemuorodhesha kama kocha msaidizi, lakini alisajiliwa akiwa kocha mkuu.
“Imeshatokea, acha niwe mkweli mimi nilishindwa kukaa katika benchi kwa sababu jina langu kwenye usajili wa Caf lilienda nikiwa kama kocha mkuu ndio maana sikuwa katika benchi, lakini kama Hitimana angekuwepo tangu zamani mimi ningekuwa kwenye benchi,” alisema Gomes na kuongeza;
“Nikienda kwenye timu nyingine nitakaa kwenye benchi kama kocha msaidizi, wakati huu pia naendelea kusoma ila pia inanishangaza kuona leseni yangu ni ndogo kwa Caf A wakati Ulaya (hii yangu ya Uefa A) ni kubwa, inanishangaza.”
MAISHA SIMBA
Gomes anasema akiwa ndani ya Simba kwa takribani miezi 10 maisha yake yalikuwa mazuri kwa muda wote licha ya wakati mwingine kukutana na changamoto timu inapopata matokeo mabaya.
Kocha huyo anasema amekuwa na wakati mzuri na viongozi wa Simba na hajawahi kuwa na tofauti nao hivyo anaondoka huku moyo wake ni msafi kwa ajili ya kutafuta changamoto mpya.
“Simba ujue ni timu kubwa hapa na ukiwa kocha wake lazima ujivunie kuwa hapa, kiukweli najivunia kuwa kocha wa Simba lakini upande mbaya kwangu kwa hivi karibuni ilikuwa ni baada ya kufungwa na Yanga kwenye mchezo wa ufunguzi wa ligi.”
UKUTA KUTOBADILIKA
Wadau wa soka nchini wamekuwa wakihoji kwanini mabeki Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Pascal Wawa na Shomari Kapombe wakati mwingine wanaonekana kuchoka lakini bado wamekuwa wakiendelea kupewa nafasi.
Gomes ameweka wazi sababu zilizomfanya aendelee kuwaamini wachezaji hao akisema: “Sidhani kama wamechoka, Kapombe kwa ukweli ni mchezaji mzuri sana. Tangu msimu uliopita amekuwa na wakati mzuri hata akiwa na timu ya Taifa, sidhani kama ni mchezaji mbaya, ila muda mwingine huwa anapotea tu kidogo kwenye mchezo na hii ni kawaida kwa mchezaji yeyote,” anasema Gomes na kuongeza;
“Wawa ni mchezaji mzuri katika eneo la kati na nimekuwa nikiongea naye, hata jana (juzi) niliongea naye kuhusu hali yangu ya kuondoka nikamuambia aendelee kupambana, alilia sana. Nilijaribu kumtuliza na kumrudisha katika hali yake.”
UBINGWA UKO PALE PALE
Gomes amewaonya wapinzani wa timu hiyo ya Msimbazi akisema licha ya kuanza msimu kwa kusuasua na pia kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, bado timu hiyo ndiyo yenye nafasi kubwa zaidi ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa nara ya tano mfululizo msimu huu na pia kutisha Afrika kupitia Kombe la Shirikisho.
“Simba ina kikosi kizuri na hata ukiniuliza namna ambavyo tumetolewa siwezi kupata jibu la wazi, lakini huko walipo bila ya shaka wataingia fainali na nina imani kubwa katika hilo,” anasema Gomes na kuongeza;
“Hata kwenye Ligi Kuu ya hapa pia Simba wana nafasi kubwa zaidi ya kuchukua tena ubingwa, nadhani kuanzia mchezo wa Polisi (wa juzi) wakipata matokeo mazuri na katika mechi nyingine chache zinazofuata, Simba itatulia na kurejea kwenye hali yao ya ushindi.”
Gomes anasema Simba wanaweza kuchukua ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika miaka ijayo lakini jambo kubwa ambalo wanatakiwa kulifanya ni kuendelea kuwaweka pamoja wachezaji wao.
Kocha huyo anasema Simba hawakatazwi kuwauza wachezaji wake lakini wanapofanya hivyo wanatakiwa walete wachezaji wengine ili kuendelea kufanya vizuri na kufika fainali.
“Kama Simba wanataka ubingwa wasiuze nyota wao, wakikaa kwa pamoja muda mrefu na kuungana bila shaka watachukua ubingwa na kuwa timu tishio hapa Afrika zaidi ya sasa,” anasema Gomes na kuongeza;
“Wachezaji waliosajiliwa kwasasa wengi wao bado wanaendelea kukua hivyo wakija wakaungana na wale waliokuwepo bila shaka watakuwa tishio na hilo lipo wazi.”
MKUDE AJIPANGE
Gomes anasema amezungumza na Jonas Mkude na kumwambia kuwa anatakiwa kufanyia kazi kipaji chake kama anataka kuwa mchezaji mzuri zaidi na kupata nafasi katika kikosi cha Simba.
“Mkude namuamini na naamini katika uwezo wake na kipaji, lakini ili uweze kufikia malengo unatakiwa kutumia muda mwingi kufanya mazoezi utafika mbali zaidi ya hapa ulipo sasa, kama amenielewa na kukubaliana na kauli yangu nina imani atakuwa bora na ataisaidia Simba,” anasema Gomes na kuongeza;
“Suala la kucheza kwenye kikosi cha Simba bado lipo kwenye mikono yake yeye mwenyewe Mkude.
“Lwanga (Tadeo), Sadio (Kanoute), Mzamiru (Yassin) na Erasto (Nyoni) wote ni wazuri kwenye kiungo lakini kila moja ana staili yake ya kucheza.”
“Kila mchezaji nimewahi kumpa nafasi ya kucheza hii inaonyesha nilikuwa naelewa umuhimu wao kikosini, shida ni kwa Mkude ambaye sijamtumia mara nyingi hivi karibuni kwasababu hajafanya mazoezi na timu muda mrefu,” anasema na kuongeza:
“Hakuna mchezaji ambaye hakuwa na namba kwenye kikosi changu, ukiona mchezaji sijamtumia basi kashindwa kunishawishi mazoezini na amekosa moja ya programu zangu kuelekea mchezo husika.”
Credit – Mwanaspoti