Kikosi cha KMC jana kimefanya maandalizi yake ya mwisho kuelekea katika mchezo wa Ligi kuu ya NBC soka Tanzania bara dhidi ya Kagera Sugar mchezo ambao utapigwa leo katika uwanja wa Benjamini Mkapa saa 1:00 usiku.
KMC FC ambao ni wenyeji wa mchezo huo, watashuka katika uwanja wao wa nyumbani hapa Jijini Dar es Salaam kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa ligi ya NBC soka Tanzania bara Septemba 17 mwaka huu licha ya kwamba mchezo huo pia utakuwa ni wa mzunguko wa tano tangu kuanza kwa ligi hiyo.
Kikosi hicho cha wana Kino Boys hadi sasa kimeshafanya maandalizi ya kutosha na kwamba licha ya mchezo huo kuwa na ushindani mkubwa lakini malengo, mipango na mikakati ya uongozi, benchi la ufundi pamoja na wachezaji ni kuhakikisha kwamba ushindi unapatikana na hivyo kuondoka na alama tatu muhimu.
“Licha ya kuwa hatuna matokeo mazuri, lakini mashabiki zetu bado wanaendelea kuwa pamoja na sisi hivyo tunadeni kubwa kwao la kuhakikisha tunawapa burudani yenye matokeo mazuri kwenye mchezo wetu wa kesho dhidi ya wapinzani wetu Kagera Sugar”.
“Mchezo hautakuwa mrahisi lakini sisi tumejipanga kukabiliana na mazingira yoyote ya mchezo huo na kikubwa ni kuondoka na alama tatu muhimu ukuzingatia kwamba KMC ni timu kubwa na bora hivyo siku zote inapambana kupata matokeo mazuri uwanjani”. Amesema Chrsitina Mwagala, Afisa Habari wa KMC.
Hata hivyo KMC FC hadi sasa imeshacheza michezo minne ambayo ni dhidi ya Polisi Tanzania, Coast Union, Yanga pamoja na Namungo ambapo katika michezo hiyo imetoka sare mchezo mmoja, suluhu mchezo mmoja na imepoteza michezo miwili na kushika nafasi ya pili kutoka mwisho ikiwa na alama 2 wakati Kagera ipo nafasi ya 9 ikiwa na alama 5.