STAA wa Yanga kutoka Uganda, Khalid Aucho ni miongoni mwa mastaa walioitwa na Kocha Nasreedine Nabi fasta kambini na leo hii ataanza kukiwasha na wenzie kwenye gym ya Viwanja vya Gymkhana Jijini Dar es Salaam, wakitoka hapo wanapitiliza Kigamboni mchana.
Tayari tangu juzi Aucho alishaanza mazoezini binafsi gym akiwa kwao. Aucho aliumia goti kwenye mechi dhidi ya Mali na Uganda ambapo alikosa sare ya Yanga na Namungo mkoani Lindi hivikaribuni na kuibua mjadala midomoni mwa mashabiki.
Jana Aucho aliposti picha zake akiwa gym huku akishukuru daktari wa viungo na kuwaahidi mashabiki wa Yanga wamtegemee punde. Kwa mujibu wa viongozi wa Yanga, mastaa wote akiwemo Aucho watakutana na Nabi Gymkhana bila kukosa na jioni watafanya mazoezi ya Uwanjani tayari kwa mchakamchaka wa kujiandaa na mechi ya Mbeya Kwanza ugenini wiki ijayo.
Yanga inarejea kambini baada ya mapumziko ya siku moja ikitoka kwenye sare iliyoibua mijadala mitandaoni kutokana na matukio mbalimbali yaliyojitokeza ndani ya dakika 90 ikiwemo yale ya penalti.
Kocha wa Yanga, Nesreddine Nabi ameliambia Gazeti la Mwanaspoti kwamba anajua kilichotokea Lindi na nini cha kurekebisha. Yanga imedondosha pointi mbili za kwanza katika mechi zake sita walizocheza mpaka sasa,wakiwalazimisha wenyeji wao Namungo juzi kwa sare ya bao 1-1 katika Uwanja wa Ilulu ambao historia Yanga inaonyesha unawasumbua kwa miaka mingi.
Nabi ambaye ana uraia pacha wa Ubelgiji na Tunisia, alisema; “Tulipokwenda kwenye mazoezi ya mwisho nilishtuka niligundua tutakuwa na dakika 90 ngumu kutokana na ubora mdogo wa uwanja ni uwanja mwingine mbovu sana niliuona hapa Tanzania, hatukuwa na muda tena wa kutafuta akili ya mbadala kwa kiwango tulichotakiwa kufanya.”
“Naamini tutarudi na nguvu zaidi baada ya kuzipoteza pointi 2,tutabadilika na kurudi kwa nguvu. Timu yetu haikucheza katika ubora ambao tulicheza hapo nyuma lakini tunatakiwa kujifunza na hili tunatakiwa pia kujiandaa kwa ubora wa viwanja vya namna hii, ”alisisitiza Kocha huyo.
Alisema akili yao sasa ni Mbeya kwanza utakaopigwa tena ugenini Uwanja wa Sokoine Mkoani Mbeya wiki ijayo akisema anaamini pia atakuwa amewapata wachezaji wake wote.
“Tuna siku za kutosha kurekebisha yote ambayo yalitupa changamoto lakini pia wapo wachezaji ambao tuliwakosa kutokana na maumivu nafikiri wakati huu watakuwa wako sawa,” alisema Nabi ambaye anasaidiwa na Mrundi, Cedrick Kaze. Yanga katika mchezo dhidi ya Namungo walimkosa kiungo wake muhimu, Aucho ambaye alipata mchubuko wa goti akiwa na Uganda. Akizungumzia utata wa penalti ambayo iliwapa sare hiyo Nabi alisema hataki kuingia katika migongano na wanaosimamia ligi lakini akakumbusha jinsi kikosi chake kilivyowahi kunyimwa bao mkoani humo.
“Hata kama nina mtazamo wangu kuhusu tukio lile,siruhusiwi na kanuni lakini naona kama kuna namna ya watu kuona Yanga inakwama, tuwaachie wasimamizi.”