Home Makala BAADA YA ‘KUWASHIKA HASWA’ YANGA…AUCHO ASHINDWA KUJIZUIA..UFUNGUKA KUHUSU DILI LAKE NA SIMBA

BAADA YA ‘KUWASHIKA HASWA’ YANGA…AUCHO ASHINDWA KUJIZUIA..UFUNGUKA KUHUSU DILI LAKE NA SIMBA

 


YANGA imecheza mechi tano za Ligi Kuu Bara msimu huu na muda huo ukatosha kuweka wazi nani staa katika kikosi hicho kilichoongezewa mastaa 10 wapya msimu huu.

Mmoja wa mastaa hao ni kiungo Khalid Aucho kijana mmoja mwenye mwili uliokolea mazoezi na kimo cha kuridhisha akitumia mguu wa kushoto kuonyesha kipaji chake.

Alipofika Yanga alianza kufanya kazi yake katika mchezo wa Ngao ya Hisani na hapohapo akausafisha uongozi wa klabu yake kwamba jamaa ni kiungo sahihi ambaye Bilionea mfadhili wa klabu hiyo Ghalib Said Mohamed ‘GSM’ kutumia fedha zake kumsajili. Mwanaspoti limefanya mahojiano maalum na juu ya maisha ya soka ya raia huyo wa Uganda;

AUCHO NI NANI?

“Historia ya maisha yangu kuielezea inaweza kuhitaji kama wiki kuimaliza lakini kifupi mimi ni mzaliwa wa Uganda katika eneo linaloitwa Jinja mashariki,nimezaliwa mwaka 1992,unajua hilo eneo ni kama tumebarikiwa kuna vipaji vingi nami ni mmoja wao na nimepitia katika timu za taifa na sasa bado niko hapo,nimeanzia mpira katika shule za soka nikakua hivyo mpaka sasa.”

MAISHA MAPYA YANGA

Aucho anasema hakuna shida kabisa na kwamba anachofanya ni kuhakikisha anakuwa na maisha mazuri na yenye furaha ndani ya klabu hiyo.

“Maisha ndani ya Yanga ni mazuri hata kama nitakutana na changamoto kitu muhimu ni kuondoa changamoto na kurudi katika maisha mazuri, napenda kuwa mtu mwenye furaha kwahiyo furaha lazima unapokutana na changamoto unaiondoa na kuwa sehemu unayotaka,” anasema Aucho.

WACHEZAJI WAMEMPOKEAJE

Aucho anafurahia mapokezi yake kutoka kwa wachezaji wenzake ndani ya Yanga akisema:”Nafurahi tangu nimeingia hapa nipo vizuri na wachezaji wenzangu na hata viongozi kila kitu kinakwenda vizuri kama timu inawezekana kuna wakati mambo yasiwe sawasawa kwa asilimia 100 lakini tunaishi kama familia moja kitu cha kufurahisha kila mtu yuko tayari kutoa mchango wake kwa asilimia 100 kwa ajili ya klabu yao.

YANGA KUANZA LIGI KWA KASI

“Nikweli tumeanza vizuri ligi lakini sio kitu rahisi hasa unapopambana na timu zilizo nyuma yenu kila moja inakuja ikitaka kupunguza kasi yenu, kwahiyo inakuwa ni mapambano makubwa, sisi tunazihitaji pointi lakini jambo zuri tuko katika kikosi kinachojitambua majukumu yake, kitu muhimu tunatimiza kile ambacho makocha wetu wanataka tukifanye na mwisho tumefanikiwa kushinda hizi mechi.

ANAGUSA ANAACHIA

Kama umemuangalia Aucho akiwa uwanjani kitu ambacho kimewakosha wengi ni jinsi anavyopiga pasi zake kwa haraka akiwa hana mambo mengi akisema huwa hataki shida akitambua mpira una kasi zaidi yake.

“Maisha yangu huwa sipendi mambo magumu lakini pia sipendi kufanya mambo yawe magumu kwa wengine, ninachofanya ni kufanya kila kitu kuwa rahisi nje na ndani ya uwanja, ndio maana mnaniona nacheza mpira wa pasi moja au mbili kwasababu nataka kufanya mambo kuwa rahisi ili yaende.

“Unajua kitu ambacho mimi nafahamu mpira una kasi zaidi yangu kwahiyo sitaki kukimbia nao kwa kushindana nao, ninachofanya nautumia mpira ukimbie kwa niaba yangu, binadamu hawezi kukimbia kushinda mpira, nitapiga pasi ili ikifika itajulikana Khalid amepiga.

ANAKIONAJE KIKOSI

“Yanga tuna kikosi kizuri, wachezaji kama mnavyowaona ni wenye vipaji vikubwa, ukiangalia kwa nidhamu hujasikia kama kuna shida kila mmoja anataka kuonyesha kipaji chake ili asaidie klabu kwahiyo timu iko vizuri na naamini tunaweza kufikia malengo ya klabu kwa msimu huu kama tukiendelea kuwa kama tulivyo sasa.

“Unajua kuna wakati kama uko sehemu kama timu na mkawa tayari kufanya kazi kila kitu kitakwenda vizuri na kama pia kutakuwa na uwezeshaji mzuri kitoka kwa uongozi wa klabu na hiki ndio kipo hapa Yanga.

LIGI NGUMU KIASI GANI

“Ukiangalia tunashinda sio maana kwamba ligi ni rahisi itakuwa ngumu kama tukipoteza,hakuna timu rahisi ambayo inakuja uwanjani kupoteza ushindani upo mkubwa lakini kitu muhimu kwetu kama Yanga ni kuangalia mechi zetu na kutafuta ushindi kwa ajili ya malengo yetu.”

MATAJI YANAKUJA

Yanga inapita katika msimu wa tano bila kuchukua taji lolote kubwa ukiondoa lile la Mapinduzi la msimu uliopita lakini Aucho anaamini hiyo ni ndoto yake na klabu kwa ujumla na kwamba inawezekana.

“Ni ndoto yangu lakini pia ni ndoto za klabu na ni malengo yetu na hiki ndio kinachotufanya tupambane ukiniuliza mimi hiki ndio kitu ambacho kimenileta hapa Yanga ni kuhakikisha nashinda mataji, binafsi naona inawezekana kwa aina ya ubora wa timu yetu, nimeambiwa kwamba kuna muda hapa klabu haijachukua mataji kwahiyo hili li deni kubwa kwetu.

SOMA NA HII  HUYU HAPA MFARANSA MRITHI WA MIKOBA YA KAZE YANGA

ALIWAHI KUHITAJIWA NA YANGA KABLA YA SASA?

Miaka fulani nyuma kuliwahi kuenea uvumi kwamba Aucho anakuja Yanga wakati huo akiitumikia Gor Mahia kumbe ukweli ulikuwa hivi.

“Nakumbuka tulikuja hapa na Gor Mahia sikumbuki kulikuwa na mashindano gani hapa kama nakumbuka vizuri ilikuwa ni cecafa, tulipokutana na Yanga tukawafunga mabao mawili, baada ya hiyo mechi nikawa naona taarifa kwamba Simba na Yanga zinanihitaji na wengine wakasema nimeshasaini lakini hakukuwa na ukweli na hakukuwa na klabu ambayo ilikuwa imenifuata kwahiyo sikuona shida ya kuanza kusumbua akili yangu katika hilo.”

SAFARI YA KUJA YANGA KUTOKA MISRI

Yanga ilimsajili Aucho akitokea klabu ya El Makkasa ambayo alisitisha nayo mkataba na hapa anaelezea jinsi uhamisho huo ulivyokuwa.

“Uhamisho wangu kutoka Makkasa kuja hapa nadhani ulikuwa rahisi niliamua kusitisha mkataba baada ya kuona kuna mambo hayako sawa na hawakutaka kukubali nikaona niwashtaki Fifa na sababu kubwa walikuwa hawanilipi nikaona siwezi kuendelea kuteseka wakati nacheza na napambana lakini hakuna ninachopata kwahiyo uamuzi wangu ukawa huo na sasa nipo Yanga,” anasema kiungo huyo mwenye nguvu na mwili uliojengeka kimazoezi.

 NI AZAM NA YANGA SIO SIMBA

“Nilikuwa nasikia uvumi kwamba nilikuwa natakiwa pia na Simba kuwa nakwenda Simba, ukweli ni kwamba sikuwa na ofa yoyote na Simba na wala hakuna kiongozi wao ambaye alinipigia mimi na nikaongea nao.

“Ukweli ni kwamba nilikuwa na ofa mbili tu Tanzania nilikuwa nahitajika na Azam, niliongea nao na tukafikia sehemu lakini ya pili ni Injinia (Hersi Said) huyu ndiye niliyeongea naye sana na nikaona mambo yanakwenda sawa na mwisho tukakubaliana na nikaja kusaini hapa Yanga.

“Baada ya mazungumzo mengi na makubaliano nikaona nije Yanga na uamuzi wangu wa kuja Yanga ulitokana na kuhitaji changamoto mpya ambayo niliiona hapa patakuwa sehemu sahihi kwangu.”

ALIUMIA KUKOSA LIGI YA MABINGWA AFRIKA

Aucho hakucheza mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika ambazo Yanga walifungwa nyumbani na ugenini dhidi ya Rivers United ya Nigeria katika hatua ya awali, na kama hufahamu basi ukweli ni kwamba jamaa aliumizwa na hatua hiyo kuliko hata wachezaji wenzake ambao walicheza na sababu ni hii.

“Ni kweli sikucheza hizo mechi. Nikiwa nyumbani na timu ya taifa, nilianza kuambiwa hizo taarifa kwamba kuna uwezekano nisicheze haya mashindano nilishtuka, lakini nilisisitiza kifanyike chochote ili nicheze na baadaye nikaambiwa mambo yameshindikana hapo ndio niliumia zaidi,” anasema Aucho.

“Unajua nilikuwa na malengo makubwa katika mashindano haya na inawezekana hii ndio ilikuwa hatua muhimu kwangu kuja Yanga nilikuwa nataka kukamilisha malengo yangu makubwa na inawezekana watu hawajui umuhimu wa haya mashindano mimi kucheza mashindano makubwa kama haya kiu yangu haishii tu kucheza kuna kitu kikubwa huwa nataka kukifanya kwa faida ya timu na maisha yangu binafsi kwahiyo niliumia sana hasa unapoona timu inahitaji kitu ulichonacho usaidie wewe unacho lakini huwezi kufanya kitu, nafikiri kipo kinachohitajika kujifunza.”

NAFASI GANI ANAYOCHEZA HASA?

“Nafurahia kucheza nafasi zote za kiungo napenda kucheza kama kiungo mkabaji hii ndio nafasi ninayoitaka sana lakini inapotokea kuna mtu ambaye anaweza kufanya kazi nzuri ya kukaba vizuri hapo naweza kuanza kutembea juu zaidi kwasababu kama napata mtu ambaye anaweza kuweka ulinzi katika safu ya ulinzi hapo naweza kusogea juu sasa ikitokea nikaona hayuko vizuri nitamwambia wewe sogea juu mimi nitabaki chini.

“Unajua mimi sio mtu ambaye napenda kutanguliza kufunga napenda kwanza timu iwe salama na wengine wafunge, sitaki kutamani kufunga kisha tukapoteza, ni bora tuwe 0-0 na baada ya hapo tupate goli hapo tutakuwa tuko salama kuliko mimi kufunga halafu tukafungwa zaidi.

ANAPENDA KUCHEZA NA KIUNGO GANI?

Tangu amekuja Aucho amekuwa akicheza sambamba na Yannick Bangala na hapa anaeleza anachotamani: ”Nafurahia kucheza na kiungo yeyote ambaye kocha ataamua kunipanga naye awe Bangala, Mukoko, Mauya, Feisal na wengine kitu muhimu najua kujibadilisha ninapopangwa kucheza na yoyote kati yao hao na kitu kizuri ni kwamba wote ni wachezaji wazuri,” anasema Aucho.

Credit :- MWANASPOTI