Home news MAAJABU YA ‘FEI TOTO’ YANGA…ASIMULIA MAUJANJA YA HATARI…AJITENGENEZEA UFALME MPYA JANGWANI..

MAAJABU YA ‘FEI TOTO’ YANGA…ASIMULIA MAUJANJA YA HATARI…AJITENGENEZEA UFALME MPYA JANGWANI..


ACHANA na kina Khalid Aucho, Yannick Bangala na Fiston Mayele wanaoimbwa na mashabiki wa Yanga, kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ naye amewasapraizi Wanayanga kwa soka tamu na mabao ya kusisimua, akijitengenezea ufalme Jangwani tofauti na ilivyotarajiwa.

Fundi huyo wa mpira ambaye alitua Yanga kama kiungo mkabaji na sasa kutumika kama kiungo mshambuliaji ameuanza msimu kwa kishindo, kwani kama hafungi yeye, basi ujue atahusika na mabao ya Yanga na namba hazidanganyi buana!

Katika mechi tano ilizocheza Yanga katika Ligi Kuu Bara, Fei amefunga mabao matatu akiwa ndiye kinara wa timu hiyo na kuasisti moja akianza kufunga dhidi ya Kagera Sugar kisha alifunga bao la pili dhidi ya KMC akipiga shuti kali kama alivyofanya dhidi ya Ruvu Shooting juzi jijini Dar es Salaam.

Mabao matatu aliyonayo sasa Feisal ni pungufu na mawili aliyofunga katika msimu mzima uliopita katika mechi 34 za Yanga alipotupia kambani matano, hivyo kuonyesha wazi kama ataendelea na moto huo atafanya maajabu makubwa katika Ligi Kuu Bara.

Juu ya bao lake la juzi, Fei Toto alisema siku zote anapokuwa nje ya boksi huwa anaweka akili na macho yake katika lango la mpinzani na mpira unapofika huwa na kazi moja tu kuhakikisha anapata mpira na kuupiga ili kuifungia timu yake bao.

“Niliangalia kabla ya kuupiga mpira, nikamuona kipa amekaa vibaya, hivyo nilipohakikisha mpira umenifikia nikapiga shuti langoni, ndio maana nikafunga,” alisema Fei Toto.

Alisema anachofurahia ni kuona bao lake liliisaidia kuirejesha timu mchezoni na kuongeza mengine yaliyoendeleza rekodi yao ya kushinda mechi mfululizo hadi sasa katika ligi hiyo.

Bao hilo dhidi ya Ruvu limemfanya kiungo huyo kumpumulia Vitalis Mayanga wa Polisi Tanzania anayeongoza orodha ya wafungaji (kabla ya mechi za jana) akiwa na manne, akitofautiana naye moja.

SOMA NA HII  HII HAPA RODHA YA NYOTA WALIOMALIZANA NA YANGA MAZIMA