Home news KUHUSU CHAMA KURUDI TENA TZ…NI SUALA LA MUDA TU…AFUNGUKA KILA KITU..AGUSIA MKWANJA...

KUHUSU CHAMA KURUDI TENA TZ…NI SUALA LA MUDA TU…AFUNGUKA KILA KITU..AGUSIA MKWANJA WA YANGA…


 STAA wa Zambia, Clatous Chama amekiri kusikia tetesi zinazoendelea nchini Tanzania juu yake lakini akatamka kauli moja; “Muda utaongea.” Chama ambaye kwa sasa anakipiga na Berkane ya Morocco, aliuzwa huko na Simba mapema mwezi Agosti kwa zaidi ya Sh700Milioni.

Habari za uhakika  ni kwamba Simba na Yanga zote kwa nyakati tofauti zimefanya mawasiliano na wakala wa mchezaji huyo na kila mmoja ametoa dau lake na lolote linaweza kutokea muda wowote kabla pilau ya Krismasi halijaliwa.

Chama kwa mara ya kwanza tangu kuondoka nchini amenukuliwa na gazeti la Mwanaspoti  na kusema anajua na kusikia kila kinachoendelea kuhusiana na yeye kuhusishwa na kurejea nchini kwenye dirisha dogo la Krismasi.

Alisema kwamba hawezi kuingia kiundani juu ya suala hilo lakini muda utaongea. Staa huyo kipenzi cha mashabiki wa Simba amefafanua kwamba wakati mwingine huogopa kuzungumzia tetesi kwavile tafsiri huwa za namna mbalimbali. Alisisitiza kwamba kwa sasa kipaumbele chake ni familia yake kuhakikisha inakaa sawa, licha ya kutotaka kuingia kiundani zaidi katika ishu hiyo. Mkewe alifariki mwezi Juni mwaka huu na kumuachia watoto wadogo.

“Nakueleza ukweli na siwezi kuficha ukweli wa jambo hili au lingine lolote ila kila kitu kinakwenda vizuri na muda sahihi ukifika kila kitu kitakuwa wazi,” alisema Chama na kuongeza;

Gazeti la Mwanaspoti linadai kwamba Simba na Yanga kila mmoja amezungumza na staa huyo na wamemuahidi dau nono ingawa mpaka sasa hajafanya uamuzi wa mwisho.

Simba wanadai kwamba kwenye mkataba wa mauziano na Berkane kuna kipengele kinachomlazimu mchezaji kama atarudi Tanzania kuichezea Simba na si timu nyingine. Wameenda mbali na kufafanua kwamba hata kama klabu yoyote inamtaka lazima kwanza Simba iridhie.

Habari za ndani zinasema kwamba Simba wana uhakika mkubwa wa kumrejesha mchezaji huyo na hata wakienda nchini Zambia wikiendi ijayo kurudiana na Red Arrows watakutana nae huko kumalizana.

Lakini mmoja wa vigogo wa Yanga anadai kwamba ishu ya mchezaji huyo kutua Jangwani dirisha dogo iko kwenye hatua nzuri na hata wikiendi iliyopita walikuwa Kigali, Rwanda alipokuwa jukwaani timu yake ikicheza na APR ya huko.

SOMA NA HII  WAKATI BODI YA LIGI WAKIIKATALIA SIMBA KUCHEZA NA COSTAL...MBRAZILI KAAMUA KUJA NA GIA HII...

Yanga wanadai kwamba staa huyo hayuko tayari kurejea Msimbazi kutokana na presha aliyoipata mpaka kukubali kuondoka ingawa Berkane hapati nafasi ya kucheza kama ilivyokuwa Simba.

KWANINI HACHEZI?

Chama alisema hali ya hewa ya Morocco siyo mbaya sana ila ipo tofauti na Tanzania alipopazoea kutokana kuna baridi na hata utamaduni wao ni mpya kwake lakini anaweza kuzoea kidogo kidogo kadri muda unavyokwenda.

Chama alisema kutokucheza ndani ya Berkane mara kwa mara ndio maisha ila bado hajazoea timu na wachezaji wenzake.

Anaamini baadae atapata nafasi ya kucheza zaidi kwani katika kipindi kifupi kilichopita alipata majeraha na yalimrudisha nyuma.

“Nikirudi katika kikosi naweza kufanya vizuri, timu na wachezaji wenzangu najitahidi kuwazoea,”alisema Chama ambaye Mwanaspoti linajua amewaambia watu wake wa karibu kwamba anataka kuondoka Berkane.

“Ligi ya Tanzania na ya Morocco tofauti yake mpira ni ule ule ila viwanja na mipango mingine wameendelea na wapo juu ila maeneo mengine yanafanana,”

“Kila mchezaji anaweza kucheza aliyetoka Tanzania anaweza kucheza ligi ya Morocco mengine ni changamoto tu,kwa wakati huu siwezi sana muda utaongea.”

Mmoja wa viongozi wa Simba alidai kwamba Yanga itakwama kwa Chama kwani wao bado hata hawajalipwa fedha yote ya mauzo na Berkane; “Jambo lingine ambalo watu wa Yanga hawafahamu Chama usajili wake tulitakiwa kupewa Dola 320,000 ambazo ni zaidi ya Sh700 milioni na hawakutupatia yote bado tunawadai Dola 100,000 ambazo ni zaidi ya Sh320 milioni.”

“Kwahiyo hizo taarifa kuwa anakwenda Yanga labda Chama mwenyewe atudanganye kwani hatuwezi kumlazimisha maamuzi yake tofauti na hayo ya kutuhakikishia yupo tayari kurejea Simba kama RS Berkane tutakubaliana nao,”aliongeza kiongozi huyo wa Simba. Msimu uliopita alitwaa tuzo ya kiungo bora.