SIMBA haitaki masihala kabisa, ni baada ya kutangaza bonasi ya Sh 1Bil kuwapa wachezaji wao kama wakifanikiwa kuwafunga watani wao, Yanga katika Kariakoo Dabi.
Hiyo ikiwa ni siku chache tangu mabosi wa Yanga watangaze bonasi ya Sh 1Bil kama wakifanikiwa kuwafunga Simba katika dabi hiyo inayotarajiwa kupigwa Jumamosi hii saa 11:00 jioni kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu Bara.
Katika kuelekea mchezo huo, Yanga wataingia uwanjani wakiwa vifua mbele baada ya kuwafunga Simba bao 1-0 katika mchezo uliopita wa Ngao ya Jamii, ambalo lilifungwa na Mkongomani, Fiston Mayele.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano, Bodi ya Wadhamini wa timu hiyo chini ya mwenyekiti wake, Abdallah Salim ‘Try Again’ kwa kushirikiana na mwekezaji wao, Mohammed Dewji ‘Mo’ wametenga kiasi hicho cha fedha ili kufanikisha ushindi.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa, bodi hiyo walifanya kikao cha haraka cha kuweka mikakati ya kuelekea dabi hiyo mara baada ya mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Red Arrows uliochezwa juzi huko Zambia.
Aliongeza kuwa wameweka kiasi hicho cha bonasi kwa ajili ya kuongeza morali na hali ya kujituma katika mchezo huo unaotarajiwa kujaa upinzani mkubwa.
“Uongozi unafahamu umuhimu wa mchezo huu dhidi ya Yanga, siyo mwepesi ni mchezo unaovuta hisia za watu wengi ambao unaingia kwenye rekodi, hivyo ni lazima tushinde.
“Kuchukua ubingwa wa ligi pekee haitoshi, kuwafunga ni muhimu, hivyo maandalizi yamekamilika na tupo tayari kwa ajili ya mchezo huo.
“Viongozi wamefanya kikao tayari mara baada ya mchezo wa shirikisho dhidi ya Red Arrows, hivyo akili na nguvu zao wamezielekeza katika dabi, wametoa ahadi ya Sh 1Bil kama bonasi ya wachezaji kama wakiwafunga Yanga,”alisema mtoa taarifa huyo.
Katika kuelekea mchezo huo, Try Again alisema kuwa: “Gari la Simba hivi sasa limewaka baada ya kuwaondoa Red Arrows, nguvu na akili zetu tunazielekeza katika mchezo ujao wa ligi ambao ni muhimu kwetu kushinda.”