HAWATAAMINI! ni tambo za wanachama wa Yanga ambao wamejinasibu kuibuka na ushindi dhidi ya wapinzani wao Simba kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa Uwanja wa Mkapa.
Hayo yamesemwa na wanachama wa Tawi la Mtoni Mtongani kwa kile walichodai kuwa kiungo na mshambuliaji wa timu hiyo Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Fiston Mayele watawaliza Simba mapema.
Mjumbe wa tawi hilo, Said Maulid (SMG) alisema kuwa kuelekea mchezo huo hawana presha na wapinzani wao maana kwa sasa wanaishi kwa kuunga unga tu.
“Nawasikitikia ndugu zetu, wengi tunajua mechi hizi huwa hazitabiriki lakini hata kipindi ambacho tulikuwa wabovu hawakuweza kutufunga sembuse sasa ambapo tuna wachezaji tishio kila eneo,” alisema.
Kauli ya SMG iliungwa mkono na mjumbe wa tawi hilo Said Mohamed ‘Gaucho’ akisema kuwa Simba watafungwa mapema kutokana na ubora wa kikosi chao msimu huu.
“Tuna Mayele, Fei Toto hao ni trela tu wako wengine wengi sasa wanatokaje kwa mfano, yaani tutakachowafanya Simba ni kuwadhalilisha tu siku hiyo,” alisema.
Naye mjumbe wa tawi hilo Msafiri Kandula alisema wameanza vizuri Ligi msimu huu hivyo wanachokifanya ni kuendeleza wimbi la ushindi.
“Kinachonipa imani ya kushinda ni wachezaji tuliokuwa nao, wanajituma wana ari mwanzo mwisho tofauti na wenzetu ambao hawana uhakika wa kupata matokeo,” alisema.
Mjumbe mwingine wa tawi hilo Idd Said alisema timu hiyo imekamilika kuanzia kwao mashabiki na wachezaji hivyo anawaomba mashabiki wao kujitokeza kwa wingi kuipa sapoti timu yao.
“Yanga ya msimu huu ni mwanzo mwisho hakuna anayeweza kutushusha pale juu, wapinzani wetu wajiandae kisaikolojia maana tunaenda kuongeza wigo wa pointi” alisema.
Tawi hilo lilianzishwa mwaka 2021, lina wanachama 190, viongozi ni Mwenyekiti Yusuph Bakari, msaidizi wake Omary Mbile, Katibu Mkuu Juma Fundisha, msaidizi wake Ramadhan Jamal, Mtunza fedha Fikiri Hassan ‘Gereza’.