UNAAMBIWA Simba wamekuja na staili ya kata mti panda mti, hii ni baada ya kuchukua maamuzi ya kuachana na kiungo mshambuliaji wao Mmalawi, Duncan Nyoni na kumalizana na kiungo Mzambia, Samuel Sikaonga.
Nyoni aliungana na Simba mwanzoni mwa msimu huu, kwa mkataba wa miaka mitatu, akitokea Silver Strikers ya Malawi, lakini ameshindwa kuonyesha kiwango bora ndani ya timu hiyo jambo linalodaiwa kuwapelekea mabosi wake kumfungashia virago.
Chanzo chetu kutoka Simba, kimesema, kwamba, baada ya uongozi wa Simba kujadiliana kwa kina matakwa ya ripoti ya Kocha Mkuu Pablo Franco, umelazimika kukatisha mkataba na Nyoni ili utoe nafasi kwa kiungo Samuel Sikaonga.
“Ripoti ya kocha Pablo imeleta mabadiliko na maamuzi mazito sana ndani ya Bodi ya Wakurugenzi, hasa upande wa kamati ya usajili, ambapo umekata majina takriban matatu ya nyota wetu na kuachana nao rasmi akiwemo Nyoni.
“Kocha hajaridhishwa na uwezo wa Nyoni, jambo ambalo ameipa kamati ya usajili kutafuta mbadala wake, ambapo wao wameamua kumng’oa rasmi na kuingiza jina la Sikaonga ambaye atahudumu moja kwa moja katika nafasi ya Taddeo Lwanga,” kilisema chanzo hicho.
Alipotafutwa Ofisa Mtendaji Mkuu (C.E.O) wa Simba, Barbara Gonzalez, ambaye simu yake ilikuwa haipokelewi hadi tunakwenda mitamboni, lakini mmoja wa vigogo wa Simba, ambaye hakutaka kuwekwa wazi alilithibitishia kuwa kweli wameshaachana rasmi naNyoni.