PAPE Sakho ameiongoza Simba kipindi cha kwanza dhidi ya Selem View katika mechi yao ya Kombe la Mapinduzi hivyo kwenda mapumziko ikiwa kifua mbele kwa bao 1-0.
Mechi hiyo inachezwa Uwanja wa Amaan kisiwani hapa ambapo Simba imeonekana kulishambulia zaidi lango la wapinzani wao huki kipa Beno Kakolanya akiwa hana kashikashi nyingi langoni kwake.
Sakho aliifungia Simba bao la kuongoza dakika ya 25 akipokea krosi ya John Bocco na kupiga mpira uliomshinda kipa wa Selem View, Yussuf Abdu Ali.
Katika kipindi hicho cha kwanza Simba ilifanya mashambulizi mengi langoni mwa wapinzani wao ingawa nao hawakuonekana kuwa makini sana kwenye unaliziaji.
Bocco alijaribu kupiga shuti dakika ya 13 lakini kipa Ali aliipangua shuti hilo na hata dakika ya 32 kiungo Hassan Dilunga naye alikosa bao baada ya shuti lake kupigwa pembeni mwa goli.
Simba ilikosa mabao mawili ambalo lilipigwa na Bocco pamoja na Pascal Wawa baada ya mwamuzi wa mchezo huo Mohamed Simba kukataa mabao hayo kwamba waliotea.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi , ambapo ni Simba tena kupitia kwa kiungo wake Rally Bwalya aliiandikia goli la pili kwa shuti kali la umbali wa mita ishirini, na kumshinda mlinda mlango wa Selem View.
SHIBOUB AINUA MASHABIKI
Wakati mechi hiyo inaendelea kipindi cha kwanza kocha wa Simba Pablo Franco alimwamsha Sharaf Shiboub kwa ajili ya kupasha ambapo mashabiki walionekana kufurahishwa na uwepo wake.
Shiboub alionyesha ishara ya kuwasalimia ndipo mashabiki waliinuka na kumshangilia huku wakimpigia makofu kwa shangwe.