HATIMAYE Mshambuliaji wa Zanaco FC ya Zambia, Moses Phiri, amefungukia dili lake la kujiunga Yanga, huku akiweka wazi kuwa bado hajamalizana rasmi na klabu hiyo.
Phiri raia wa Zambia, kabla ya kuhusishwa na Yanga, alikuwa akihusishwa kujiunga na Simba ambao awali walionesha nia ya kumsajili kabla ya upepo kuhamia Yanga.
Akizungumza moja kwa moja kutoka Zambia, Phiri alisema japo uongozi wake umefanya mazungumzo na Yanga, lakini bado hajasaini mkataba wa kuitumikia timu hiyo, hivyo ataendelea kuwa mchezaji wa Zanaco.
“Mazungumzo na Yanga yalifanyika kati ya uongozi wangu na uongozi wa Yanga, lakini hayakukamilika kwa kuwa timu yangu bado inahitaji niendelee kucheza hapa, hivyo bado nitaendelea kuitumikia Zanaco FC.
“Kama kuja Tanzania nitakuja Juni, mwaka huu ambapo ligi itakuwa imemalizika. “Ukiachana na Yanga, kuna timu nyingine tatu kutoka Tanzania ambazo zinanihitaji, hivyo tutaona itakavyokuwa,” alisema Phiri.
Wakala wa Phiri, Nawa Nyambe, alizungumzi hilo kwa kusema: “Yanga wametutafuta kuhusu Phiri, lakini Zanaco wapo kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho na tunapendelea acheze kwenye mashindano haya makubwa.
“Atapata uhamisho wake, lakini anahitaji kutumikia mkataba wake na Zanaco, tutaanza kuangalia ofa kuelekea mwisho wa msimu.”
Baada ya kutokea hilo, mmoja wa viongozi wa Yanga, ameliambia Spoti Xtra kwamba: “Tumepata taarifa za Zanaco kuzuia Phiri kujiunga na Yanga katika usajili huu wa dirisha dogo, lakini kama uongozi hilo suala tumelipokea vizuri.
“Mmoja wa viongozi wetu (Injinia Hersi Said) alikuwepo nchini Zambia, hivyo tunaamini watakuwa wamefikia muafaka mzuri na Zanaco ambayo imemzuia kuondoka hivi sasa.
“Hivyo tunaamini tutafikia muafaka mzuri na Phiri atasaini Yanga kama siyo katika dirisha dogo, basi lile dirisha kubwa.”