Home news NKANE ATISHWA NA SIMU ZA YANGA…MRISHO NGASA AMCHANA WAZI KUHUSU ‘MADEM, NA...

NKANE ATISHWA NA SIMU ZA YANGA…MRISHO NGASA AMCHANA WAZI KUHUSU ‘MADEM, NA STAREHE’..


WINGA wa zamani wa Yanga, Mrisho Ngassa aliandika ujumbe mzito kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Instagram, kumtaka nyota mpya wa timu hiyo, Denis Nkane kujituma kwa bidii na baadaye kumuendea hewani kabisa, lakini kinda huyo amesema ukiacha simu hiyo ya hamasa, zilimiminika nyingine nyingi hadi zikamtisha, akajifungia.

Nkane alisemakwamba, amezungumza kwa kirefu na Ngassa kwa njia ya simu na alimshauri kuwa mwangalifu na jiji la Dar es Salaam, lililo na mambo mengi yanayoweza kuhatarisha kipaji chake.

“Amenishauri vitu vingi, ameniambia anatamani kuona naendeleza alipoishia yeye Yanga, nifanye makubwa kuliko aliyoyafanya yeye, anatamani nikifanikiwa kuvaa jezi yake itajwe kwa kiwango kizuri na siyo udhaifu,” alisema Nkane na akaongeza kuwa;

“Ameniambia mengi kuhusu maisha ya jiji la Dar es Salaam hasa baada ya kujiunga na Yanga, ikiwemo namna ya kuepukana na vishawishi vitakavyoua ndoto zangu, akanisisitiza kwamba ameyaona hayo na hataki yanikute,” alisema.

Aliulizwa jezi namba 16 aliyokuwa anavaa Ngassa kama yupo tayari kuitumia? Akajibu: “Wakati nakua nilikuwa nakwenda kwenye vibanda vya kuonyesha mpira Yanga ikicheza kumwangalia Ngassa, nipo tayari kuliendeleza jina lake kupitia jezi hiyo pia kujiendeleza mimi mwenyewe.”

Jambo jingine aliloambiwa na Ngassa ni kwamba atakuwa anamfuatilia katika mechi zake na kumpa moyo.

“Nimefarijika na maneno yake, sikujua kama kaka yangu Ngassa angeweza kunikalisha chini na kunitakia mema katika hatua nyingine ya maisha yangu ya soka,” alisema.

MAPOKEZI YA YANGA

Nkane alizungumzia mapokezi yake Yanga yalivyomuachia deni analotakiwa kulilipa kupitia mguu wake uwanjani.

“Kiukweli mapokezi yamekuwa makubwa, yameniongezea ari ya kujituma kwa bidii na kunipa picha ya namna watu wanavyoona kipaji changu kwa ukubwa huo, nimebakiwa na deni ninalotakiwa kupambana kulilipa,” alisema Nkane na kuongeza;

Nkane alisema ameshangazwa na jinsi ambavyo amepigiwa simu nyingi na watu tofauti, jambo ambalo halijawahi tangu aanze kucheza soka.

“Yaani sijawahi kuona simu nyingi kama hizo, zilinifanya nibakie ndani muda mrefu, kwani nikawa naogopa hata kutembeatembea mtaani, naomba Mungu anisaidie kazi yangu iwe ile waliyoitegemea ama zaidi ya hiyo,” alisema.

SOMA NA HII  GAMONDI WA YANGA NAE ATAMBA, AWATAJA MASTAA HAWA KATIKA USAJILI WA MSIMU HUU