Meneja wa Idara ya Habari ya ya Simba SC Ahmed Ally amewapoza Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo baada ya kupoteza mchezo dhidi ya Kagera Sugar jana Jumatano (Januari 26).
Simba SC ilikua mkoani Kagera kucheza mchezo huo wa kiporo na kuambulia kichapo cha 1-0, ambacho kinaendeleza machungu yaliyoibukia mjini Mbeya juma lililopita na kisha mkoani Morogoro.
Simba SC ilipoteza dhidi ya Mbeya City kwa kufungwa 1-0 na kuambulia sare ya bila kufungana dhidi ya Mtibwa Sugar juma lililopita.
Ahmed ametumia ukurasa wake wa Instagram kuwasisilisha ujumbe wa kuwatuliza Mashabiki na Wanachama wa Simba, huku akiwatia moyo kwa kuwaaminisha timu yao itarudi kwenye kipindi cha neema na furaha.
Ahmed Ally ameandika: Tunapitia kipindi kigumu.. tutakaa sawa, ni suala la muda @simbasctanzania kurejea kwenye ubora wetu
Asante Kagera Sugar kwa upinzani na hongereni kwa ushindi..
Poleni mashabiki wetu tunajua mnapitia wakati mgumu lakini haya ndo maisha ya mpira.
Tunarudi nyumbani kwenda kuangalia tumekosea wapi ili turudi imara zaidi bado safari ni ndefu muhimu ni kutopoteza focus.
Simba SC imebaki na alama zake 25 zinazioweka nafasi ya pili kwenye msimamo, huku ikiachwa na Young Africans kwa tofauti ya alama 10.
Kagera Sugar imechupa hadi nafasi ya tisa wakitokea nafasi ya 11 kwa kufikisha alama 16.