KITENDO cha kipa namba moja wa Yanga, Djigui Diarra kuwa kwenye majukumu ya taifa lake, kimempa ujiko Abdultwalib Mshery kuonyesha umahiri wake, unaomfanya Kocha Nesreddine Nabi kuwa na uhakika wa ulinzi.
Mshery baada ya kusajiliwa Yanga akitokea Mtibwa Sugar, alifikia majukumu ya kudaka mechi dhidi ya Dodoma Jiji, Coastal Union na Polisi Tanzania na zote hajaruhusu bao.
Mwanzo wa Mshery umekuwa mzuri, nje na kuwa na mabeki wanaomsaidia ulinzi, pia kuna hatari ambazo zilifika moja kwa moja golini kwake na aliziokoa.
Kiwango alichokionyesha kipa huyo, kimemuibua kipa wa zamani wa timu hiyo, Benedict Haule aliyesema, ameonyesha ukomavu licha ya umri wake kuwa mdogo.
“Mshery kaanza kishujaa, hilo linamwondolea hofu kocha, anapokosekana Diarra bado timu yake inakuwa salama, dogo anafanya kazi nzuri anastahili kupongezwa,” alisema.
Kwa upande wa kocha wa makipa, Idd Pazi alisema anapoona vijana wa umri wa Mshery wanaonyesha kujiamini ndani ya klabu kongwe, anapata faraja ya kuona tegemeo Stars.
Pazi ambaye alizifundisha Simba, Moro United alisema Mshery ni kipa mzuri, anayeweza kuanzisha mashambulizi kama Diarra, hivyo kinachotakiwa kwake ni uzoefu wa kuendana na maisha ya Yanga.
“Simba na Yanga zina maisha tofauti na timu nyingine, namaanisha malengo yao ni ubingwa tu, hivyo lazima ajue mazingira hayo, ili ikitokea timu ikapitia magumu ajue namna ya kukabiliana nayo,” alisema.