Home news PAMOJA NA LIGI KUWA BADO SANA….HIVI NDIVYO YANGA ‘WALIVYOIKALIA SIMBA KIMTINDO’

PAMOJA NA LIGI KUWA BADO SANA….HIVI NDIVYO YANGA ‘WALIVYOIKALIA SIMBA KIMTINDO’


VITA ya Simba na Yanga ni kwenye ushindani wa kila jambo, kama upande huu unacheka, kesho utalia na mwingine unapokea furaha, hivyo siyo vitu vya kushangaza ndani ya klabu hizo.

Mfano mzuri ni namna msimu ulioisha (2020/21), mashabiki wa Simba walitembea vifua mbele, lakini 2021/22 kufikia sasa mambo yamegeuka, Yanga kunaonekana kumenoga zaidi, huku Msimbazi ikipitia wakati mgumu wa kusaka raha.

Bado ligi ni ndefu, lakini katika raundi 13 tayari klabu hizo, zimeonyesha ubabe wa mechi za nyumbani na ugenini, zinazowafanya mashabiki wao wacheke na kununa.

Mwanaspoti linakuchambulia michezo iliyochezwa na Simba na Yanga kwa njia ya takwimu ujue walichovuna katika michezo ya nyumbani na ugenini.

Mechi za nyumbani Yanga imecheza 5, imefunga mabao 12 na iliruhusu mabao mawili na pointi 15, Wakati ugenini imecheza michezo 8, sare 2, imefunga mabao 11, imeruhusu mabao mawili na kukusanya pointi 20.

Yanga inaongoza kileleni kwa pointi 35, kutokana na chati iliyoonyesha kwa mechi za nyumbani na ugenini.

Mechi 6 ilizocheza Simba nyumbani, imeshinda 4, sare 2 sawa na pointi 14, imefunga mabao 6 imeruhusu bao 1, Ugenini kabla ya mechi ya jana kule Kagera, Simba ilikuwa imecheza mechi 6, ushindi 3, sare mbili 2, kupoteza 1, pointi 11, mabao 8, na kuruhusu mabao manne.

Kutokana na mwenendo wa timu hizo, beki wa zamani wa Yanga, Oscar Joshua anaiona taswira ya ubingwa inakwenda Jangwani.

“Mfano msimu ulioisha Yanga, ilifungwa na Coastal Union, msimu imeifunga mabao 2-0, ilitoka sare na Polisi Tanzania, imefunga bao 1-0, hiyo inaonyesha ni namna gani msimu huu ina jambo lake,” alisema.

Kauli ya Oscar inakinzana na mtazamo wa kocha wa zamani wa Gwambina FC, Athuman Bilali ‘Bilo’ aliyesema bado ligi ni ndefu na lolote linaweza kutokea.

“Ligi yenye ushindani huwezi kutabiri Yanga ni bingwa, nakumbuka msimu ulioisha Yanga iliongoza lakini Simba (japo ilikuwa na viporo vingi tofauti na mwaka huu), ikapindua meza, lolote linaweza likatokea kama ubingwa kwenda Jangwani ama Msimbazi, acha muda uongee,” alisema.

SOMA NA HII  PAMOJA NA KUANZA VYEMA SIMBA...PABLO ASHINDWA KUJIZUIA..AFUNGUKA MSIMAMO WAKE...

Beki wa zamani wa Yanga na Stars, Samson Mwamanda alisema wanachotakiwa kukifanya mastaa wa timu hiyo ni kukaza na kupata ushindi wa mabao mengi, utakaoinyong’onyeza Simba.

“Wachezaji wanatakiwa kujua mashabiki ama klabu inataka nini kwao, si mchezo miaka minne kukosa ubingwa.”