Uamuzi wa Kampuni ya GSM kujiondoa katika udhamini mwenza wa Ligi Kuu Bara umepokewa kwa hisia tofauti na klabu mbalimbali huku Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) likikiri kuondoka kwa wadhamini hao.
Juzi jioni, GSM kupitia kwa Ofisa Biashara Mkuu, Allan Chonjo ilisema kuwa wameamua kujiondoa kutokana na TFF pamoja na Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) kushindwa kutekeleza vipengele vya kimkataba wa miaka miwili ambao pande hizo mbili zilikubaliana.
“Haya hayajawa maamuzi rahisi kwa kampuni ya GSM kwani tunatambua zipo baadhi ya klabu za mpira zitaumizwa pamoja na wadau mbalimbali na hatua hii haikuwa dhamira yetu kufikia uamuzi huu mgumu,” alisema Chonjo.
“Upande wa klabu udhamini wa tutaendelea kuwa kwenye mkataba wetu kama kawaida bali tumejitoa upande huu wa ligi.”
Mbali na kujitoa katika udhamini wa ligi, mmiliki wa kampuni hiyo, Gharib Said naye amejiondoa kwenye kamati ya ushindi ya timu ya taifa ‘Taifa Stars’.
Muda mfupi baada ya GSM kutangaza kujitoa, TFF ilithibitisha kupokea barua ya uamuzi huo na kuahidi kuufanyia kazi.
“Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linathibitisha kuwa leo Februari 7, 2022 limepokea barua ya kuvunja mkataba wa mdhamini mwenza (co – sponsorship) wa Ligi Kuu ya NBC kutoka kampuni ya GSM.
“TFF inafanyia kazi barua hiyo na itatoa taarifa kwa wadau wa mpira wa miguu kuhusu suala hilo,” ilisema taarifa ya TFF.
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, viongozi wa klabu za soka wameonyesha kutofautiana kwa kilichotokea.
Mwenyekiti wa Mtibwa Sugar, Nassor Abubakar alisema timu yao inaendeshwa kitaasisi na haitegemei sana wadhamini, hivyo kujitoa kwa GSM hakuwezi kuwayumbisha.
“Sina maana kwamba pesa za udhamini hazitusaidii, ila kuondoka kwa GSM hatuwezi kuyumba kwani ni tasisi inayojitegemea.” alisema Abubakar.
“Kuhusu nembo ya GMS kwenye jezi tunasubiri Bodi ya Ligi na TFF ambavyo ni vyombo makini kutupa taarifa rasmi na mwongozi wa nini tufanye baada ya hapo.”
Kwa upande wake, Ofisa Habari wa Ruvu Shooting, Masau Bwile alisema kitendo cha GMS kujitoa udhamini mwenza wa ligi ni maumivu makubwa kwao, kwani walitarajia pesa hizo kuwasaidia kiuendeshaji.
“Japokuwa bado hatujapokea taarifa rasmi, nimeona kupitia mitandao ya kijamii, inaumiza kwani tayari tulianza kuweka mabango uwanjani, nembo kwenye jezi na sijui sababu haswa za maamuzi yao ni nini,” alisema Masau.
Makamu Mwenyekiti wa Polisi Tanzania, Robert Munisi alisema wamepokea kwa masikitiko taarifa za GSM kujiondoa udhamini mwenza wa ligi, kwani tayari walishauingiza kwenye bajeti yao.
“Kuondoka kwao kumevuruga bajeti yetu. Mbaya zaidi ni katikati ya msimu, jambo ambalo litaumiza vichwa vyetu,” alisema Munisi.
Naye Katibu wa Kagera Sugar, Masoud Ally alisema kujiondoa kwa GSM kutayumbisha timu kiuchumi kwa kuwa tayari walishawasaidia.
Mkataba wa GSM na TFF ulisainiwa Novemba mwaka jana hivyo umedumu kwa siku 76.