Home news YANGA,BIASHARA NA RUVU WAMZIKA SONSO….MANARA AIBUA ZOGO MSIBANI…ADAI BINADAMU WANAJEURI…

YANGA,BIASHARA NA RUVU WAMZIKA SONSO….MANARA AIBUA ZOGO MSIBANI…ADAI BINADAMU WANAJEURI…


Klabu za Yanga, Biashara United na Ruvu Shooting zimejitokeza kumsindikiza mchezaji Ally Mtoni Sonso ambaye amezikwa saa 10 jioni  kwenye makaburi ya Ndugumbi jijini Dar es Salaam.

Wachezaji na viongozi wa klabu hizo waliwasili  kwa nyakati tofauti nyumbani kwa wazazi wa Sonso mtaa wa Mzumbe, Magomeni Kondoa.

Biashara United ndio ilikuwa timu ya kwanza kufika msibani hapo na kukaa kwa dakika chache na nusu saa baadae kuaga kwa madai walikuwa na mechi jioni.

Meneja wa Biashara United, Frank Wabare, amesema wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo Cha Sonso na wanamtakia pumziko jema uko aendako.

“Biashara United tumepokea kwa huzuni msiba huu kwani licha ya kwamba hajawahi kucheza timu yetu lakini ni mwenzetu kwa sababu alikuwa akishiriki ligi ambayo tupo. tunamuombea Mungu ampumzishe kwa amani, ” amesema Wabare.

Wabare alikabidhi rambirambi ya sh 500,000 kwa familia ya marehemu.

Baada ya kuondoka Biashara United , wachezaji na viongozi wa Ruvu Shooting, alikokuwa aliichezea marehemu waliwasili kuhani msiba huo.

Msemaji wa Ruvu Shooting, Masau Bwire amesema kama timu wamepata pigo kuondokeaa na Sonso lakini wanamshukuru Mungu kwa yote na wanamuombea uko aendako.

Masau alikabidhi rambirambi ya sh1 milioni kwa ajili ya msiba huo.

Baada ya Masau kumaliza kuongea, ndipo akakaribishwa msemaji wa Yanga, Haji Manara ambaye aliibua kelele kwa watu wengi waliohudhuri msiba huo kila mmoja alitaka kumuona.

Wachezaji wa Biashara United, wakiwa msibani nyumbani kwao marehemu Ally Sonso, mtaa wa Mzunbe Magomeni Kondoa.

Manara amesema  Sonso alikuwa mchezaji mwenye nidhamu  aliyekuwa na sifa ya kucheza kwa jihadi uwanjani bila kumuogopa yoyote.

“Yanga tulimsajili Sonso kutoka Lipuli mwaka 2019 na moja ya sifa yake kubwa ni kucheza kwa jihadi ,mpiganaji ndani ya uwanja, huwa hacheki na mtu na nidhamu yake ndani ya timu haina mfanona hii iwe funzo kwa wachezaji vijana.

“Jambo la kufurahisha ni kwamba alivyocheza tu klabu kubwa Afrika Mashariki na Kati (Yanga) ndio alipata nafasi ya kuitwa timu ya Taifa lakini timu nyingine zote alizopitia ikiwemo ya Masau Bwire hajawahi kupata nafasi hiyo ,” amesema Manara na kuwavunja watu mbavu.

SOMA NA HII  KUHUSU ISHU YA WAWA KUTEMWA AU AACHWE...PAWASA AIBUKA NA HILI..ATOA ONYO KALI...

Manara amesema  wanadamu tuna jeuri kwa sababu tuna pumzi, na afya njema lakini sisi wote hatuijui siku yetu hivyo wote tunapaswa kujiandalia mwisho mwema.

Amesema kwa niaba ya mwenyekiti wa klabu ya Yanga, wajumbe wa kamati ya utendaji, wachezaji na mashabiki wanatoa pole kwa  familia na wadau wote walioguswa na msiba huo na kama klabu wametoka sh1 Milioni ya rambirambi.

Wakati akitoa rambirambi hiyo Manara aliwavunja watu mbavu tena baada ya  kuuliza Ruvu wametoa shilingi ngapi na alipojibwa kuwa sh1 Milioni  alisema haiwezekani wanatakiwa kuongeza kwani msiba ni wao huku yeye akimwambia Masau Bwire atamuongezea sh 200,000 kuongeza katika rambirambi yao kwani anajua wana hali ngumu.

Pia katika msiba huo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi kila mmoja akitoa rambirambi ya sh1 milioni.

Mchezaji Elias Maguri wa Ruvu Shooting  amesema wamepokea kwa masikitiko makubwa msiba wa Sonso na watamkumbuka kwa mengi.

“Tulipopata taarifa ya msiba tulishtuka na kuahirisha. Tumeishi nae vizuri tumesikitika na tunandelea kumuombea apumzike kwa amani,” amesema Maguri.

Naye mchezaji wa Biashara United, Atupele Green amesema kama wachezaji wamesikitshwa na msiba huo na wanamuombea Sonso apumzike kwa amani.

” Bado alikuwa anahitajika kutokana na umri wake lakini kazi ya Mungu Haina makosa.Kifo hiki kiwe funzo kwetu kujiandaa muda wowote kwani hatujui siku wala saa ya kutwaliwa, ” amesema Atupele.