IKIWA ni miezi miwili tangu akabidhiwe mikoba ya Milton Nienov, kocha mpya wa makipa wa Simba, Tyron Damons kutoka Afrika Kusini amechambua mwenendo, Aishi Manula na Benno Kakolanya akisema kila mmoja kivyake katika uchezaji.
Tofauti na macho ya wengi yanayotazama makipa wakiokoa michomo au kumaliza mchezo bila nyavu zao kuguswa pekee kwa Msauzi huyo kwake ni tofauti kabisa anawatazama vile wanachangia upatikanaji wa mabao.
Tyron alisema siku hizi soka limebadilika, makipa ndio wamekuwa wa kwanza kuanzisha mashambulizi, hivyo pua zao zinatakiwa kunusa kwa haraka na macho yao kuona nafasi (mikimbio) ambazo zinaweza kutengenezwa.
“Nafurahia viwango vya makipa wangu, tumekuwa tukifanyia kazi mambo kadhaa ambayo naamini yatawafanya kuwa bora zaidi, kipa sio kudaka tu wanatakiwa kuuelewa mchezo unahitaji nini, anaweza kuwa chanzo cha kuuamua,” alisema Tyron na kuongeza;
“Wakati mpira ukiwa mikononi unatakiwa kujua wapi unatakiwa kwenda, kwa kufanya hivyo itarahisisha mwendo kwa timu kushambulia, lakini akiwa na maamuzi ya kuchelewa hutoa nafasi kwa wapinzani kujipanga.”
Akijikita kwa kuwazungumzia, Aishi na Kakolanya wanaocheza mara kwa mara kikosini, alisema ni aina mbili tofauti ya makipa na kila mmoja ana ubora wake wa kuusoma mchezo.
“Beno ni mzuri sana pale ambapo timu inafanya shambulizi la kustukiza, hucheza na akili za washambuliaji, Manula uwezo wake ni mkubwa kuanzisha mashambulizi kuanzia nyuma,” alisema Tyron.
Tyron mwenye umri wa miaka 43 ana Diploma C na D ya Shirikisho la Soka Afrika pia ameshiriki kozi mbalimbali za ukipa kama KVBN, SAFA na Evolution Conference iliyofanyika nchini Uingereza.
Kabla ya kujiunga na wekundu hao wa Msimbazi alikuwa kocha wa makipa wa Chipa United inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini, pia aliwahi kufundisha TS Galaxy 2018/19 na Bidvest Wits.