USHINDI wa mabao 3-1 nyumbani umewapa mzuka zaidi viongozi wa Simba na sasa katika kujipanga kuhakikisha wanaendeleza kasi hiyo ugenini dhidi ya USGN ya Niger na ile ya RS Berkane ya Morocco umempa kazi maalumu Clatous Chama.
Simba ilianza vyema mechi zake za makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Asec Mimosas ya Ivory Coast katika mechi iliyopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam na Jumapili watavaana na USGN mjini Niamey, Niger.
Katika kuhakikisha mambo yanaendelea kuwa laini, benchi la ufundi la Simba limeamua kumtumia Chama katika mechi hizo za ugenini kwa kumjumuisha katika kikosi kinachoondoka jijini Dar es Salaam leo.
Kikosi cha Simba kinaondoka na wachezaji 24 akiwemo Chama ambaye licha ya kutokuwa sehemu ya mechi hizo kutokana na kwamba alishaichezea RS Berkane katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, lakini ana kazi maalumu ya kuisaidia timu hiyo.
Mmoja wa viongozi wa Simba amefichua kwamba, wanaondoka na Chama kwa vile ni mzoefu kwenye mechi za kimataifa na kuwahi kucheza Morocco, wakiwa na nia ya kuhakikisha wanapata matokeo mazuri ugenini.
“Tumeamua kusafiri na Chama ambaye tunatambua kabisa kuwa hatakuwa miongoni mwa wachezaji watakaocheza katika mchezo huo, ila kuna sababu za kiufundi ambazo ndizo zimetufanya kusafiri naye,” alisema mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa timu hiyo, Mulamu Nghambi.