KWA mara ya kwanza kwenye miaka ya hivi karibuni safari hii, Simba itacheza mechi ya kwanza ugenini kwa staili ya aina yake. Kutokana na ishu za usafiri hawatakuwa na ratiba ndefu Niger na watakanyaga uwanjani siku ya mchezo. Hawatakuwa na muda wowote wa kupiga tizi.
Msafara ulikwama kuondoka Dar es Salaam mchana wa Februari 17 kama ilivyokuwa imepangwa na badala yake uliondoka jana jioni na Shirika la Ndege la Ethiopia kwenda Niger kwa mchezo wao wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya US Gendarmarie (USGN) Jumapili usiku.
Hilo ni pambano la pili la Kundi D la michuano hiyo, Simba ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 3-1 iliyopata kwa ASEC Mimosas
Msafara huo utakuwa safarini kwa siku mbili wakilala mjini Addis Ababa, Ethiopia na kesho asubuhi watapita Togo kabla ya kuibukia Niamey, Niger ikiwa ni siku moja kabla ya kuvaana na wenyeji wao ambao wana rekodi nzuri nyumbani.
Katika msafara huo huenda wakaondoka na kiongozi mmoja Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’ pamoja na muwakilishi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ahmed Mgoyi.
Jopo na viongozi wengine wa Simba akiwemo Ofisa Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez wataungana na kikosi hicho Morocco siku mbili kabla ya kuvaana na RS Berkane na wameamua kufanya hivyo kutokana na mzunguko wa safari kuwa mrefu.
Kuondoka kwa Simba leo maana yake watafika usiku Niger, siku moja kabla ya mchezo na watapata muda wa kupumzika, hawatafanya mazoezi katika kiwanja cha mechi kama ilivyo kawaida ya timu ngeni.
Jambo hilo linaweza kuipa wakati mgumu Simba ambao inaenda kwa mara ya kwanza nchini humo, hivyo kutojua mazingira ya nchi hiyo japo tayari ilishatuma watu mapema kuweka mambo sawa kabla ya timu kutua mjini Niamey.
Kocha Mkuu wa Simba, Pablo Franco alikiri hilo linaweza kuwasumbua, japo bado anawaamini vijana wake, imewatokea kama dharura tofauti na mipango ya awali.
“Hali kama hii tulikutana nayo wakati tunacheza mechi tatu za Ligi Kuu dhidi ya Mbeya City, Mtibwa Sugar na Kagera Sugar zote tulikuwa ugenini tulilazimika kusafiri bila ya kupata muda wa kufanya mazoezi na kujiandaa kucheza michezo hiyo migumu na vitu vyote hivyo ndani ya siku tisa tu,” alisema Pablo na kuongeza;
“Kutokana na mahitaji ya timu hatuna jinsi kukabiliana na hali ilivyo na kwenda ugenini kupambana kutafuta pointi katika mechi zote mbili zilizo mbele yetu ingawa tunafahamu itakuwa ngumu.”
Wakati huo huo Pablo alisema taarifa alizokuwa nazo siku moja kabla ya kusafiri wachezaji wanne hawatakuwa sehemu ya kikosi, Hassan Dilunga atakayekuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na jeraha lake la goti.
Pablo alisema ana imani Dilunga atarejea katika majukumu yake punde, Rally Bwalya yupo kwao Zambia alikopata msiba, Chriss Mugalu na Kibu Denis wanaendelea na matibabu.
“Kutokana na yalivyo mashindano haya ni ngumu kushinda mechi mbili ugenini ila tunaendelea kuandaa timu kutokana na muda huu mchache ili kuona tunapata kile ambacho tunahitaji,” alisema Pablo na kuongeza;
“Hatuna tena muda wa kufanya mazoezi lakini maandalizi yetu ya awali na yale ya kiakili kwa wachezaji naimani yamekuwa vizuri kwa kiasi kikubwa kulingana na wapinzani walivyo vile tulivyo waona.”
Kocha wa zamani wa Biashara Unted, Francis Baraza amewaonea huruma Simba na kusema; “Mtazamo wangu Simba hawatakuwa na shida na watacheza vizuri katika mechi hiyo na kushindwa kwao labda mbinu zao ziwe si imara kama wapinzani wao lakini kwa maana ya umbali wa safari watakuwa na muda wa kupumzika.”