WAWAKILISHI wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho Afrika Simba wamefanikiwa kupata sare ya bao 1-1, ugenini dhidi ya USGN ya Niger.
USGN wenyeji wa mchezo walikuwa wa kwanza kupata bao dakika 12, kupitia kwa Gbeuli Wilfried baada ya uzembe wa wachezaji wa Simba.
Bao hilo lilitokana na makosa ya beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ pamoja na Sadio Kanoute aliyekuwa wa mwisho kupoteza mpira mpaka bao kupatikana.
Katika kipindi hicho cha kwanza Simba walikuwa imara katika kuzuia licha ya kupokea mashambulizi ya mara kwa mara na kufanya makosa lakini hawakufungwa bao zaidi ya hilo.
USGN kupitia kwa washambuliaji wake walitengeneza nafasi za mara kwa mara ila walishindwa kuliona lango la Simba pengine kutokana na ubora wa wachezaji wa Simba ikiwemo kipa, Aishi Manula.
Katika kipindi cha pili Simba walirudi vizuri hawakufanya makosa katika eneo hilo la ulinzi na walitengeneza nafasi za kufunga ingawa hazikuwa hatari kama zile mbili za Meddie Kagere na moja ya John Bocco.
Mabadiliko waliyoyafanya Simba kuingia Bocco na Benard Morrison yalionekana kuwa na tija katika kikosi hicho na kufunga bao la kusawazisha.
Morrison aliyeingia dakika 65, kuchukua nafasi ya Yusuph Mhilu aliweza kuifungia Simba bao la kusawazisha dakika 83, kwa kichwa baada ya kuunganisha kona ya Shomary Kapombe.
Morrison kabla ya kufunga bao hilo ambalo lilikuwa muhimu kwa Simba ilitokana na kufuata mpira kama anataka kupiga kona lakini alipokwenda kwenye boksi alikutana na mpira huo na kuunganisha kwa kichwa.
Baada ya kupata bao hilo la kusawazisha Simba walishangilia kwa furaha yote na kurudi uwanjani wakicheza kwa nidhamu kubwa na kulinda sare hiyo waliyofanikiwa.
Baada ya mechi Simba walikwenda kuwa vinara wa kundi hilo wakiwa na pointi 4.
Matokeo mengine katika kundi hilo ‘D’ Asec Mimosas walishinda nyumbani kwao mabao 3-1, dhidi ya RS Berkane ya Morocco.
Kwa matokeo ya mechi zote hizo Simba ndio vinara wa kundi pointi 4, Mimosas nafasi ya pili tatu sawa na Berkane wakati USGN ndio wanaburuza mkia na pointi moja.