UNAAMBIWA Simba hawajataka kumuacha nchini kiungo wao mshambuliaji, Clatous Chama, wakiwa na sababu zao ambazo zimesababisha wasafiri naye licha ya kwamba hawezi kucheza katika michuano hii ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Chama hana ruhusa ya kucheza katika michuano hiyo akiwa na Simba kwa kuwa tayari ameshaitumikia RS Berkane katika michuano hiyo, jambo ambalo Caf hawaruhusu mchezaji mmoja kucheza katika timu zaidi ya moja kwa msimu mmoja.
Meneja wa Habari na Mawasiliano ya Simba, Ahmed Ally, aliweka wazi kuwa waliamua kusafiri na Chama kwa kuwa watakuwa nje ya nchi kwa muda mrefu, hivyo anatakiwa afanye mazoezi na timu.
Sababu nyingine ambayo Ahmed alisema iliwafanya wasafiri na kiungo huyo Mzambia, ni kuwasaidia katika mchezo wao dhidi ya timu yake ya zamani ambayo ni RS Berkane ya Morocco.
“Kuhusu Chama kusafiri naye kila kitu kipo wazi kuwa tutakuwa nje ya nchi kwa muda mrefu zaidi ya siku 10, hivyo ni ngumu kwa mchezaji kukaa siku zote hizo bila kufanya mazoezi, jambo ambalo limesababisha na yeye awe huku ili apate muda wa kufanya mazoezi na wenzake.
“Lakini pia tutacheza mchezo wetu wa pili dhidi ya RS Berkane tukiwa huko Morocco, Chama anawafahamu vizuri kwa kuwa amewahi kucheza pale, kuna vitu vingi nadhani atatusaidia katika mchezo huo japo hatacheza,” alisema Ahmed.