MWENYEKITI wa Baraza la Wazee la Simba, Hassan Dalali amefunguka kuwa anatamani kikosi chao kikutane na Yanga kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC) ili wajitengenezea mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa wa kombe hilo kwa mara ya tatu mfululizo.
Simba wana uwezekano mkubwa wa kukutana na Yanga kwenye kombe hilo endapo timu hizo zitashinda mechi zake za robo fainali. Simba wamepangwa na Pamba huku Yanga wakitarajiwa kucheza na Geita Gold.
Mzee Dalali ameliambia gazeti la Championi Jumamosi, kuwa: “Nina imani tutapata matokeo kwenye mechi ya robo fainali ili tuweze kutinga hatua ya nusu fainali na tunawaombea wenzetu Yanga wapate matokeo dhidi ya Geita ili tukutane nao kwenye hatua ya nusu fainali tuwafunge vizuri.
“Msimu wa 2020 tuliwafunga mabao 4-1 kwenye nusu fainali pia msimu uliopita tuliwafunga kwenye mchezo wa fainali kule Kigoma, hivyo Yanga ni timu ambayo tumeifunga mara nyingi kwenye michuano hii na tunatamani pia tukutane nao kwenye hatua ya nusu fainali ili tuendeleze ubabe dhidi yao.”