Kuelekea mechi kati ya Geita Gold FC dhidi ya Yanga unaotarajiwa kuchezwa Jumapili ya Machi 6 katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza mashabiki wa timu hiyo wamewalalamikia uongozi wa timu kwa kudai kuuza mechi na hawajatendewa haki mchezo kupelekwa Mwanza.
Mashabiki hao wamedai uongozi wa timu uliwaahidi kuwa mechi za mzunguko wa pili zitafanyika katika uwanja mpya wa Geita lakini wanashangazwa kwa mechi kupelekwa Mwanza huku mashabiki wa timu wakiwa Geita.
“Mimi ni shabiki lakini siwezi kwenda Mwanza uwanja wa Nyankumbu ni kama wa Manungu sasa kwa nini wapeleke Mwanza hapa usalama upo na mechi zinachezwa leo nini kimewafanya wapeleke mechi Mwanza kama sio kuuza mechi” alidai Alipha Zuberi.
“Huu ni ujanja ujanja umefanyika sisi hatuendi tena kama wao wamepeleka Mwanza basi wakatoe mashabiki Mwanza wawashangilie timu ndogo zikija tunaujaza uwanja leo wameona timu kubwa wameona wahamishie mchezo huu ni ujanja wa kuuza mechi”
Amesema mechi hiyo ingechezwa Geita ingeleta fursa za kiuchumi kwa wakazi wa Geita “Hii ni fursa kwa watu wangeuza chakula, bodaboda wangepata pesa na hata sisi wa stendi tungesafirisha abiria lakini wao viongozi wameamua kupeleka mechi Mwanza” amesema Zuberi
Akizungumza malalamiko hayo katibu mkuu wa Geita Gold FC Simon Shija amewataka mashabiki wa timu hiyo kutosikiliza uvumi unaoendelea katika mitandao ya kijamii kuwa mechi imeuzwa kwakuwa sio kweli na wanachotafuta wao ni kupata alama tatu za ushindi.
Shija amesema mechi yao na Yanga imepelekwa Mwanza kwa sababu za kiusalama kwa kuwa uwanja wa Nyankumbu hauwezi kumudu mashabiki wa timu zote mbili lakini pia wamezingatia suala la usalama kwakuwa uwanja ule ni wa shule ya wasichana.