YANGA inazidi kupasua anga ikionyesha inalitaka kombe na wakati mbio hizo zikiendelea kocha wao Nesreddine Nabi ameshusha mkwara mzito akiwachonganisha mastaa wake wakiwamo Saido Ntizbazonkiza, Fiston Mayele, Djigui Diarra, Khalid Aucho, Fei Toto na wengine kwamba hakuna mwenye uhakika wa namba kikosini, isipokuwa kwa yule tu anayefanya makubwa tu kushinda wenzake.
Vinara hao wa Ligi Kuu Bara wakikusanya jumla ya pointi 42 katika mechi zao 16 za msimu huu, wakiwa pia ndio timu pekee ambayo haijapoteza mechi yoyote hadi sasa, wanatarajiwa kuondoka kwenda jijini Mwanza kuwahi pambano lao la ligi hiyo dhidi ya Geita Gold litakalopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Jumapili hii, lakini kabla ya safari hiyo itakayofanyika jana Ijumaa, Kocha Nabi aliamua kufunguka mambo kadhaa ikiwamo vita ya namba kwa vijana wake.
Nabi alisema wakati wakiifuata Geita Gold kuwa kuna mastaa wake kama wawili au watatu wanarejea katika kikosi chake ambao wanakuja kuleta vita mpya ya nafasi.
Nabi alisema beki wake wa kati Dockson Job aliyesimamishwa mechi tatu anarejea kazini akiwa hana majeraha, kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ naye anarudi kazini kufuatia kuukosa mchezo uliopita kwa kuwa na kadi tatu za njano huku pia winga Chico Ushindi akirudi kazini baada ya kupona majeraha.
Nabi alisema wakati wachezaji hao wakirejea wanakutana na wengine ambao walikuwa wanacheza huku nao wakionyesha ubora mkubwa kwa kikosi chao kusimama imara katika mechi zilizopita ambapo sasa wanatakiwa kupambana kila mmoja kuwania nafasi upya.
“Wapo wachezaji ambao wanarejea tunaweza kuwa nao katika mechi ijayo ambao wana ubora mkubwa lakini shida wanakuja kukutana na wenzao ambao katika kipindi hiki wamekuwa wakifanya makubwa,” alisema Nabi na kuongeza;
“Huu ushindani wa nafasi ndio utakaotupa nafasi ya kuwa bora zaidi kwa kuwa kila mmoja atapambana kutafuta nafasi ili acheze hakuna ambaye ana uhakika wa nafasi kwamba lazima ucheze kama makocha tutaangalia kipi bora kwetu na nani yuko sawasawa.”
Akieleza zaidi Nabi alimtolea mfano Farid Mussa akisema ameonyesha ubora mkubwa tangu alipopewa jukumu la kucheza kama beki wa kushoto ambapo mabeki wa upande huo ambao wako majeruhi wanatakiwa kujipanga kwa kuwa haitakuwa rahisi kufanya uamuzi wa kumuondoa Farid.
Alisema ushindani huo anautaka pia kuonekana kwa washambuliaji wa kati ambapo sasa wanapambana kuhakikisha mshambuliaji wao aliyepoteza makali Mkongomani Heritier Makambo naye anarudisha makali ya kuja kupambana na mfungaji bora wao mpaka sasa Fiston Mayele.
“Wakati huu tunawakosa Bryson (David) na Yassin (Mustapha) ambao ni majeruhi, tumekuwa tukimtumia Farid amefanya kazi bora sana ni lazima uwe na sababu kubwa ya kumbadilisha hata kama kuna watu wamepona, watatakiwa kuonyesha kitu tofauti na huyu anayecheza sasa.
“Hiki pia tunapambana nacho kwa Makambo (Heritier) nafikiri mliona jinsi hivi karibuni tulivyokuwa tunapambana naye mazoezini ili arudi katika ubora, kama Makambo akifanikiwa kurudi katika ubora wake kutakuwa na hesabu nzuri kwa kutumika kwake na Mayele.”
Yanga iliwakosa wachezaji 9 katika mchezo uliopita wakishinda kwa mabao 3-0 dhidi ya Kagera Sugar kati ya hao majeruhi walikuwa 7 ambao ni mabeki Abdallah Shaibu , Kibwana Shomari, Bryson, Crispin Ngushi, Yacouba Songne na mawinga Ushindi na Jesus Moloko.