Dodoma Jiji imeendelea na mazoezi kwenye viwanja vya kituo cha michezo cha Filbert Bayi Kibaha, mkoani Pwani kujiandaa na mechi na Simba ya Machi 7.
Timu hiyo itakuwa ugenini kwenye uwanja wa Mkapa Dar es Salaam kucheza na bingwa huyo mtetezi wa Ligi huku kocha Masoud Djuma akipiga hesabu ya kuvuna pointi tatu kutoka kwenye timu yake hiyo ya zamani.
Mechi hiyo itakuwa ni ya pili kwa kocha Djuma kukiongoza kikosi cha Dodoma Jiji tangu alipoajiliwa hivi karibuni kuinoa timu hiyo.
Ili kuhakikisha inafanya vizuri na kurudi na pointi, benchi la ufundi la timu hiyo limelazimika kuwa na kambi ya muda mrefu ili kuzoea hali ya hewa na mazingira ya Dar es Salaam ambako kutapigwa mchezo huo wa Ligi wa mzunguko wa lala salama.
“Tuna zaidi ya wiki moja sasa tuko hapa, baada ya mechi na Ruvu Shooting hatukuondoka kurudi Dodoma, tulibaki kujiandaa kwa mechi na Simba,” amesema meneja wa timu hiyo na kuongeza.
“Hatukutaka kurudi Dodoma, kwani tulihitaji kuzoea hali ya hewa kabla ya mechi hiyo, Dodoma kuna baridi na Dar es Salaam ni joto, hivyo tumelazimika kubaki hapa Kibaha ambako hali ya hewa yake haina tofauti sana na ile ya Dar es Salaam, tunahitaji kufanya maandalizi ya kina zaidi kuelekea kwenye mchezo huo,” amesema.
Timu hiyo iliyoweka kambi jirani na kambi ya jeshi ya Msangani ina ratiba ya kujifua asubuhi na jioni kwenye viwanja vya kituo cha michezo cha Filbert Bayi, kilichopo Mkuza.
“Tulipokuja kuomba uwanja wa kufanyia mazoezi hatukufahamu kama hapa kuna mazingira rafiki ya hosteli na huduma za chakula, tulijua ni viwanja tu, ndiyo sababu tumeweka kambi pembeni kidogo na eneo ulipo uwanja tunaofanyia mazoezi ila safari ijayo tutaliweka sawa hilo,” amesema meneja huyo.
Katika mazoezi hayo, kocha Djuma alianza kwa kuwataka vijana wake kupasha kwa kukimbia kuzunguka uwanja mara tano, kisha aliigawa timu katika makundi matatu na kuwaelekeza ku control mipira na kucheza kwa mtindo wa kupiga pasi fupi fupi na kwa haraka.
Kocha huyo akiwa kwenye moja ya makundi hayo alifanya zoezi hilo lililodumu kwa dakika 20 pamoja na wachezaji, kabla ya kuwagawa wachezaji katika timu za watu wanne wanne, moja ikicheza kwa kujilinda na nyingine kushambulia na kufunga wakitumia goli moja.
Katika zoezi hilo Djuma aliwaekeza kucheza pasi za uhakika ambazo zinafika mahala huska kwa wakati.