Ally Mtoni Sonso, mmoja wa wachezaji mahiri wa Ruvu Shooting alifariki hivi karibuni jijini Dar es Salaam kwa matatizo ya mguu na Masau anaifahamu vyema stori nzima. “Sonso shida ya mguu ilianza Novemba 19, mwaka jana siku ambayo walikuwa wanacheza na Simba kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza. Saa 4 asubuhi alimfuata kocha na kumueleza anasikia maumivu ya mguu wake wa kushoto,” anasema Bwire.
Anasema ilipofika saa 8 mchana wakiwa katika maandalizi ya kwenda uwanjani, Sonso alimfuata tena kocha na kumueleza maumivu bado ni makali na anahisi dalili za mguu kuanza kuvimba.
Bwire anasema kocha alichokifanya ni kumuondoa katika orodha ya wachezaji waliotakiwa kuanza na kucheza mechi akalazimika kumuweka mwingine huku daktari akishauri abakie hotelini.
“Daktari alimshauri Sonso asiondoke ili abaki kwani pale kambini kwetu kuna hospitali yenye madaktari wenye uwezo wa kutibu na kujua matatizo ya vijana na namna ya kumsaidia. Lakini kulipokucha asubuhi siku iliyofuata, daktari anakwenda kwenye eneo lao la malazi kumtafuta ili ampeleke hospitalini kwa wataalamu ili washirikiane namna ya kumsaidia, aliambiwa mchezaji aliondoka jana muda mchache nyuma baada ya daktari wa timu kutoka.”
Masau anasema baada ya tukio hilo la Sonso kuondoka bila kuaga tofauti na walivyokubaliana walimuacha kwa kuamini amekwenda kuiona familia, mama na watoto kwani atakuwa amewamisi hajawaona kwa muda mrefu.
Anasema hawakuwa na shaka waliamini unaweza kuwa ugonjwa wa kawaida kwani lingekuwa tatizo kubwa wangejulishwa kwa kuwa wachezaji wote walikuwa majumbani kwao katika mapumziko.
“Ilikuwa Desemba Mosi nilipigiwa simu na (mke wa kocha, Boniface Mkwasa,) Betty Mkwasa aliniuliza ‘mna taarifa ya Sonso,?’ nikamjibu aliondoka hapa ila alikuwa na maumivu ya mguu sasa nadhani anaendelea vizuri kwani kungekuwa na shida tungeshajua kupitia yeye, ndugu au jamaa kwa sababu yupo kimya tuna imani yupo vizuri hana shida yoyote,” anasema Bwire na kuongeza kwamba baadaye alitumiwa picha za kutisha jinsi ulivyokuwa mguu wa mchezaji huyo.
Bwire anasema aliamua kumfuata alipo kwao Mbagala ili ampeleke kwenye matibabu Muhimbili lakini kuna vitu Sonso aliviongea kuonyesha kama hayupo tayari kwenda kupata matibabu na baadhi ya ndugu walikuwa wakisapoti.
Baada ya kumaliza kumjaza katika orodha ya wagonjwa pale Muhimbili walishauriwa kumpatia chumba cha (VIP) kwani kuna watu wengi ambao wangekuja kumuona, wakati wanataka kumchukua kumpeleka wodini Sonso alikataa na akasema hayupo tayari tena kutibiwa Muhimbili na sababu aliyoeleza tatizo alilokuwa nalo si la hospitalini na kama angedungwa sindano angeweza kupata matatizo makubwa.
Anasema wakati akiendelea na hilo la ushawishi alipigiwa simu na Boniface Pawasa ambaye alimpa taarifa ya Sonso kuitwa katika timu ya Taifa ya Ufukweni lakini alimjibu mchezaji huyu yupo Muhimbili kwa ajili ya matibabu ya shida yake lakini amegoma kutibiwa hapo. “Muda mfupi baadaye nilipokea simu ya kocha, Mecky Mexime ambaye naye alinihadithia tukio hilo linaloendelea hapo akaniambia kuna daktari anaongea naye ili aje kutusaidia.
“Baadaye katika majadiliano, mtu muhimu katika familia alitueleza kama mchezaji atatibiwa bila kuchomwa sindano sawa ila kama kuna ishu ya kumchoma sindano hawatakuwa tayari kutibiwa hapo. Ndipo ikashi-ndikana, ndugu wakaondoka naye mgonjwa nje ya hospitali kwenda kumtafutia tiba zaidi kwingi-ne.”
Bwire anasema baada ya Sonso kurudishwa nyumbani kwake kuna nyakati walikuwa wanawasiliana na Sonso au familia yake na wote walieleza anaendelea vizuri na wanatumai baada ya muda atapona kwa hiyo na wao walikuwa wanapata moyo na waliamini huko alikopelekwa kuna msaada zaidi ndio maana anaendelea vizuri.
UMAUTI ULIPOMKUTA
“Baada ya hapo sikupata nafasi ya kuongea naye tena hadi siku ya kifo chake nilipigiwa simu nikiwa kanisani Ijumaa saa 11 jioni hivi, nilipoipokea nikasikia simu ya mwanamke akilia kwa sauti na kutamka neno moja amekufa na kukata simu,” anafafanua kwa uchungu.
“Kama timu Ruvu Shooting tulishughulikia taratibu na vitu muhimu vyote vya msimu ingawa kuna watu wanatusema hatukushiriki, lakini tena tulitoa ushirikiano kikamilifu.”
SIRI YA 7-0 ZA SIMBA
Simba iliichakaza Ruvu Shooting 7-0 katika mechi yao ya 16-Bora ya Kombe la Shirikisho Azam Sports siku chache baada ya kifo cha beki huyo wa kushoto.
“Simba hii ilituotea tu maana hatukuwa sawa, tumetoka kumzika Sonso leo, siku moja tukapumzika iliyofuata tukacheza na Simba hivyo muda haukuwa mzuri kwetu, lakini machungu tukayapotezea kwa Tanzania Prisons tukawafunga kwao bao 1-0,” anabainisha.