KOCHA Pablo Franco Pablo amewachorea mbinu za kiujanja wachezaji wake ili kutetea heshima ya Simba na kuweka rekodi msimu huu. Amewaambia wachezaji wake kwamba wanachotakiwa kufanya ni kushinda kila mechi na si kufuatilia mechi za timu nyingine ili matokeo yoyote yasiwatoe nje ya mipango yao.
“Nina waamini wachezaji wangu, kama tutaendelea na mwenendo kama huu wa kila mmoja kushika kila ninachompatia katika mazoezi, tutafanya vizuri na kufikia malengo,” alisema Pablo na kuongeza;
“Tunakazi kubwa ya kufanya mbele yetu kuhakikisha tunatetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara na ushindani wa msimu huu ulivyo naamini hilo linawezekana licha ya kuwa nyuma pointi kadhaa dhidi ya Yanga.
“Hakuna anayefahamu kesho itakuwaje, kama ambavyo tulishindwa kufanya vizuri katika baadhi ya mechi na kuachwa pointi hizo, wapinzani wetu nao linaweza kuwatokea jambo kama hilo,” aliongeza kocha huyo na anaamini Simba itabeba ubingwa wa tano mfululizo wa Ligi Kuu Bara na amechora ramani ya kwenda kuing’oa Yanga kileleni.
Kutokana na kubanwa na ratiba ya mashindano mbalimbali, Pablo amepanga kufanya mambo matatu muhimu ya kiufundi yatakayokuwa na faida.
Alisema kwanza anataka kutengeneza ufiti wa kila mchezaji kuwa tayari muda wowote kucheza mechi ngumu bila ya kutetereka, kuinua viwango vya wachezaji wake ili visipishane sana kwa kuwafanya wawe na ubora unaokaribiana na la tatu ni kuhakikisha wanashinda mechi zao zote bila ya kuangalia matokeo ya wapinzani wao ili isifike wakati wowote wakajisikia kukata tamaa.
Pablo alisema ratiba yao ina mfululizo wa mechi zilizokaribiana ikiwamo hitaji la kusafiri kwa ajili ya mechi za ndani na za kimataifa za Kombe la Shirikisho Afrika, huku pia wakishiriki Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC) na Ligi Kuu, hivyo ameandaa mpango kuwawezesha kufanya vyema katika michuano yote ikiwamo ubingwa wa ligi.
“Ukiangalia wiki iliyopita tulisafiri kwa siku mbili baada ya kufika nchini tulikuwa na siku nyingine mbili tu kisha tulicheza mechi ya ligi, binafsi nachoka, unadhani kwa wachezaji inakuwaje,” alisema Pablo na kuongeza:
“Ili kukabiliana na hali hii, nahakikisha kila mchezaji hawi mbali kiuwezo, ubora na ufiti dhidi ya mwenzake, ndio maana nawatumia wachezaji wote kwa nyakati tofauti kwenye kila mechi.
“Jambo zuri kila nafasi moja kuna wachezaji si chini ya wawili, kwa mfano kuna mechi anaweza kucheza Mohammed Hussein nyingine Gadiel Michael ili kulinda ufiti wao pamoja na viwango kutokupishana.”
KUHUSU KAPOMBE
Beki wa kulia Simba, Shomary Kapombe ambaye alipata maumivu ya kichwa kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Biashara United na kushindwa kuendelea na nafasi yake kuchukuliwa na Israel Mwenda, alipata mshtuko tu.
Daktari wa Simba, Edwin Kagabo alisema: “Kapombe maendeleo yake ni mazuri baada ya vipimo alipewa muda wa kupumzika ili kuendelea kuwa sawa zaidi ila hakuna shida kubwa aliyopata.”
“Baada ya kumalizana na Dodoma Jiji, tutakuwa naye sehemu ya mazoezi pamoja na wenzake ili kuendelea na maandalizi ya ratiba yetu inayofuata.”