KOCHA Mkuu wa Simba, Pablo Franco, ameweka wazi kuwa kuelekea mchezo wao wa Jumapili dhidi ya RS Berkane, benchi la ufundi la timu hiyo linafanya maandalizi makubwa kuhakikisha si tu kwamba kikosi chao kinaibuka na ushindi dhidi ya Berkane, lakini pia kinatoa burudani ya kibingwa.
Simba wanatarajia kuvaana na Berkane kesho Jumapili katika mchezo wao wa nne wa hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika, ambapo mpaka sasa wamefanikiwa kukusanya pointi nne katika michezo yao mitatu ya awali wakishinda mchezo mmoja, sare mchezo mmoja na kupoteza mchezo mmoja.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara kwenye kundi lao D, wanakamata nafasi ya pili kwenye msimamo na pointi zao nne, huku RS Berkane wao wakiwa ndio vinara wa msimamo na pointi zao sita walizokusanya katika michezo mitatu.
kocha Pablo alisema: “Tunatarajia mchezo mgumu dhidi ya Berkane Jumapili, huu ni mchezo wa maamuzi mchezo ambao timu itakayoshinda itakuwa moja kwa moja inaongoza msimamo wa kundi hili, hivyo ni mchezo muhimu sana kwa kila mmoja.
“Lakini jambo zuri kwetu ni kuwa kwa sasa tupo katika kiwango kizuri na tutakuwa kwenye uwanja wa nyumbani, hivyo hatutacheza tu kwa ajili ya kutafuta matokeo lakini ni lazima tuonyeshe kiwango bora kama ambacho tulionyesha katika michezo yetu miwili iliyopita ya ligi kuu.”