NANI atasimama na kuwaambia Simba ukweli? Hakuna. Watu wengi wamejawa woga na hofu katika mioyo. Wanaishi kwa kudanganyana. Lakini ukweli ni kwamba wachezaji wengi Simba wamechoka na umri umekwenda. Wengi tegemeo pale Msimbazi ni wazee.
Tuanze na safu ya ulinzi. Shomary Kapombe na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ Januari, mwaka huu walitimiza miaka 30 ya pasipoti. Ndio wanaelekea katika ngwe ya mwisho ya maisha ya soka. Wanasoka wengi hustaafu miaka michache baada ya umri huo.
Katika eneo hilohilo la ulinzi, Pascal Wawa, Januari, mwaka huu alitimiza miaka 36. Ni umri wa mtu mzima. Wachezaji wengi wamestaafu kabla ya kufika umri huo. Miaka yake kwa wachezaji wa Kiafrika ni mingi mno. Yule Joash Onyango hakuna haja ya kufahamu umri. Kwa kumtazama tu anaonekana ni jua ya jioni. Umri unakimbia.
Mei mwaka huu, Erasto Nyoni atatimiza miaka 34. Nyoni ni miongoni mwa wachezaji wa Tanzania waliocheza muda mrefu. Pengine anazidiwa na Juma Kaseja pekee, lakini ukweli Nyoni ni mkongwe.
Jonas Mkude anatimiza miaka 30 Desemba, mwaka huu. Lakini ni mchezaji wa muda mrefu pia. Ni mwaka wa 12 anacheza pale Simba. Kwa miaka 10 iliyopita amekuwa panga pangua katika kikosi cha kwanza.
Nahodha John Bocco msimu huu miguu imefunga breki. Ile kazi ya kufunga iliyokuwa ikionekana rahisi mbele yake, leo hii imekuwa ngumu kama mbao za mninga. Hana goli hata moja kwenye Ligi Kuu mpaka sasa. Ni ajabu na kweli.
Pengine umri unachangia katika hili. Kwa mujibu wa taarifa za mtandaoni, Bocco anatimiza miaka 33 Agosti, mwaka huu. Ni umri mkubwa kwa mwanasoka. Bocco anacheza Ligi Kuu kwa miaka 14 sasa. Alianza kucheza 2008 na mpaka leo ni chaguo la kwanza katika timu zote alizocheza pamoja na Taifa Stars.
Meddie Kagere kwa kumtazama tu unagundua umri umekwenda. Sura na mwili wake havifichi jambo. Oktoba, mwaka huu Kagere anatimiza miaka 36. Ni umri mkubwa mno kwa mchezaji wa kutumainiwa na Simba. Ni wachezaji wachache wameendelea kuwa bora katika umri huo.
Straika mwingine, Chris Mugalu naye anatimiza miaka 32 Agostim mwaka huu. Siku zinakimbia kwelikweli.
Kwa kifupi, wachezaji wengi Simba umri umekwenda sana. Wengi jua ndio linazama katika kazi ya soka. Wengi wamecheza sana katika kipindi cha miaka 10 iliyopita. Wamechoka. Unafikiri ni tatizo kuwa na wachezaji wenye umri mkubwa? Hapana. Siyo tatizo sana kama unakuwa nao wachache. Pia katika hao wachache wasiwe tegemeo katika timu yako. Soka la kisasa linahitaji wachezaji wanaokimbia muda mwingi. Wachezaji ambao wanaweza kwenda kwa kasi kubwa dakika zote 90. Wachezaji wengi wa Simba hawawezi hili. Na ndio maana msimu huu imeanza kusuasua.
Bahati mbaya zaidi ni kwamba wachezaji wenye umri mdogo waliosajiliwa, uwezo wao sio wa kuvutia. Wengi ni wachezaji wazuri wa kawaida. Ndio maana leo hii wachezaji waliosajiliwa wengi wao bado wanakaa benchi. Yule Sadio Kanoute sio mzuri kuliko Mkude. Yule Israel Mwenda sio wa kiwango cha Kapombe. Peter Banda, Jimson Mwanuke, Yusuph Mhilu na wengineo ni wachezaji wa kawaida.
Sio wachezaji wanaoweza kuisaidia Simba kufanya vizuri na kufika fainali ya michuano ya Afrika. Ni wachezaji wazuri wa kawaida. Ubaya zaidi ni kwamba katika safu ya ushambuliaji ndipo Simba imerundika wazee wengi. Ndio maana msimu huu sio Kagere, Bocco wala Mugalu wanafanya vizuri. Wote suala la kufunga limekuwa gumu kama kucheza muziki wa singeli.
Kolamu/Makala haya yameandikwa kwanza kwenye wavuti la Mwanaspoti