Home Habari za michezo KISA BAO LAKE KUWA BORA CAF…SAKHO AVUNJA UKIMYA SIMBA…ATAKA MAKUBWA ZAIDI…

KISA BAO LAKE KUWA BORA CAF…SAKHO AVUNJA UKIMYA SIMBA…ATAKA MAKUBWA ZAIDI…


KUFUATIA bao lake alilofunga dhidi ya RS Berkane kuchagulia kuwa bao bora la wiki la Kombe la Shirikisho Afrika, kiungo mshambuliaji wa Simba, Pape Sakho, amesema habari hizo zimempa nguvu zaidi kupambana kuisaidia Simba kupata matokeo katika mchezo wao ujao dhidi ya ASEC Mimosas utakaopigwa Jumapili.

Sakho alifunga bao hilo Jumapili iliyopita katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ambapo aliwapiga chenga walinzi watatu wa Berkane akiwa ndani ya boksi lao na kupiga shuti ambalo lilimshinda kipa na kwenda moja kwa moja nyavuni.

Matokeo ya ushindi wa bao hilo 1-0 waliyoyapata Simba Jumapili yaliwafanya wakamate usukani wa msimamo wa Kundi D, la Kombe la Shirikisho Afrika.

Akizungumzia bao lake kutajwa kuwa bao bora la wiki Kombe la Shirikisho Afrika, Sakho alisema: “Nimefurahi kuona bao nililofunga kwa ajili ya timu ya Simba likitajwa kuwa bao bora la wiki la mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

“Hii ni maana halisi ya matokeo ya kupambana pamoja kama timu, pia hii ni zawadi kwa wachezaji wenzangu na Wanasimba kwa ujumla.

“Taarifa hizi zimeniongezea ari ya kupambana zaidi kwenye mchezo wetu ujao wa ugenini dhidi ya ASEC Mimosas, ili kuhakikisha tunafanya vizuri na kuweza kupata matokeo yatakayotusaidia kufika hatua ya robo fainali.”

SOMA NA HII  UKURASA WA MBELE GAZETI LA CHAMPIONI JUMATATU, USIPANGE KUKOSA NAKALA YAKO