JUZI Jumapili, AFC Leopards walipiga sare yao ya nane mfululizo baada ya kufungana mabao 1-1 na Sofapaka uwanjani Nyayo, Nairobi.
Matokeo hayo yaliwaacha katika nafasi ya 11 na kama ulitegemea kuwa kocha Mbelgiji Patrick Aussems atakasirika, basi umekosea. Mwanzo kabisa kocha Aussems ameelezea kuridhishwa kabisa na sare hizo.
Aussems anasema anabambika na droo hizo ukizingatia kuwa klabu inapitia hali ngumu ya kifedha kiasi cha kuwacheleweshea wachezaji wake mishahara yao hali ambayo imetosha kuathiri morali yao.
“Hiyo ilikuwa sare yetu ya nane mfululizo. Ukizingatia hali ngumu tunayopitia, mimi nafikiri tupo vizuri kwa sababu kwa ujumla hatujapoteza hatamara moja ndani ya mechi zetu 15 za mwisho,” Aussems katamka.
Aussem anaongeza kuwa mpango wao msimu huu ni kuhakikisha wanamaliza katika nafasi nzuri na hivyo kuwaona wachezaji wake wakijitolea kama wanavyofanya, inamridhisha sana na katu hawezi kupenda kuwasukuma zaidi.
“Haya matokeo yetu yanakuonyesha kabisa kwamba tupo kwenye fomu nzuri sana hata kama hatushindi mechi sababu ya mambo tunayopita. Haya ni matokeo afadhali yanayokuonyesha tunaweza kufanya nini kama mambo yakikaa sawa kabisa,” Aussem kaongeza.
Itakumbukwa wakati akifutwa kazi ndani ya klabu ya Simba, Aussems alisema timu hiyo haitakaa ipate matokeo mazuri tena kwa sababu inaongozwa na viongozi wajinga wajinga ambao hawana uchungu na timu.