Serikali imetilia mkazo kuwa kwa namna matumizi ya teknolojia yanavyozidi kupiga hatua hakuna kipingamizi kwamba Tanzania inahitajika kuileta teknolojia ya usaidizi wa video itakayowawezesha Waamuzi kuona matukio tata ambayo kwasasa yamekuwa yakiwaweka matatani.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema ni wazi kuwa wameyasikia malalamiko mengi yanayohusisha maamuzi yenye mkanganyiko kwenye mechi za Ligi Kuu jambo ambalo hayawafurahishiwao wakiwa ni wadau namba moja ya mchezo huo.
”Kwa hali ilivyo sasa na Teknolojia ilipofika hatuna namna tunaweza kuiepuka VAR, inawezekana tusiwenayo leo kwasababu uwekezaji wake ni gharama kubwa sana, lakini ni kitu ambacho tunakihitaji, tunajua Waziri wa fedha ni mwanamichezo na angependa hizi dosari tunazoweza kuziondoa kwa kutumia VAR zisiwepo”
“Hata mimi ni mwanamichezo nisingependa ziendelee kuwepo ,kwahivyo ni dhamira ya Serikali baadaye tunakokwenda huko kadri ya uwezo wetu ili tuwe na VAR, ili kuondoa haya malalamiko ya magoli ya mkono, goli sio goli, penati sio penati, kashika hajashika,” amesema Gerson Msigwa Msemaji Mkuu wa Serikali.