KIPA namba moja wa Simba na Taifa Stars, Aishi Manula anahesabu masaa tu ndani ya kikosi hicho kabla ya mkataba wake wa sasa kufikia tamati mwezi Juni, mwaka huu.
Manula ambaye juzi alipangua penalti mbili na michomo kibao Simba ikilala mabao 3-0 dhidi ya Asec nchini Benin, ni miongoni mwa mastaa kumi ambao Mwanaspoti linajua mikataba yao inakoma na hawajaongezwa ingawa mpango huo upo tayari.
Uongozi na kamati ya usajili wamekiri kutambua hilo na kusisitiza kwamba wanajua ni nini wanafanya, lakini vilevile wanamsikilizia Kocha Pablo Franco.
Mastaa hao ni viungo Bernard Morrison, Hassan Dilunga, Erasto Nyoni, Mzamiru Yassin, na Said Ndemla anayecheza Mtibwa Sugar kwa mkopo, mabeki Pascal Wawa, Joash Onyango na Ame Ibrahim anayekipiga pia Mtibwa kwa mkopo.
Wengine ni kipa Aishi Manula na washambuliaji Meddie Kagere na Chris Mugalu.
Awali ilielezwa Onyango alishafanya mazungumzo ya awali na mabosi wa Simba, lakini akaweka masharti yake ikiwamo kuongezewa mshahara na masilahi mengine na kuwafanya mabosi hao kurudi nyuma wakielekeza nguvu kwenye mechi za hatua ya makundi ya Shirikisho.
Mwenyekiti wa Kamati ya usajili ya klabu hiyo, Kassim Dewji bila kutaja majina ya wachezaji kiundani alisema wanatambua umuhimu wa kila mchezaji ndani ya kikosi hicho katika kuipa mafanikio timu hiyo haswa wakati huu wa kuwania kufuzu robofainali ya Shirikisho.
Alisema; “Sisi kocha ndiye mwenye kutuletea maamuzi juu ya wachezaji wake tunafanya utekelezaji tu, akisema mchezaji huyu simuhitaji hatuweza kubisha tunatafuta anayemuhitaji ili kuboresha kikosi zaidi na hiyo ndiyo kazi yetu kama kamati.”
“Sasa hivi akili zetu zipo sana kwenye michuano hii muhimu ambayo yote inatuangalia sisi, na kama mabingwa watetezi wa ligi na FA tunatakiwa kupambana zaidi, tukishamaliza haya mashindano naweza kuwa huru sasa kujikita katika usajili,” alisema Dewji ambaye ni mkongwe ndani ya uongozi wa Simba.
Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema kuwa watafanya usajili wa kishindo kwa kuongeza nyota wanne wa kimataifa.
Inafahamika kuwa tayari wameshamalizana na nyota kutoka Zambia, Moses Phiri atakayejiunga na Wekundu hao Agosti, mwaka huu na mikakati ya kumnasa Adebayor wa USGN iko pazuri.
MASTAA WASHAURI
Uongozi wa Simba umeshauriwa kulitumia vyema dirisha kubwa la usajili kwa ajili ya msimu ujao kuboresha safu zote hasa ya ushambuliaji kutokana na ukosefu wa umakini.
George Masatu ambaye ni mchezaji mkongwe alisema: “Safu ya ushambuliaji inahitaji maboresho na sio hiyo tu hata kwingine ili kuifanya timu izidi kuwa bora zaidi.”
“Inabidi mechi yao ya mwisho wajitoe sana, wasicheze kama walivyocheza jana, na Mungu anakusudi lake mchezo wa mwisho kuwa nyumbani ni fursa kwao Simba,” alisema Masatu huku akimpongeza kipa wao Aishi Manula kwa kazi kubwa aliyofanya.
Kwa upande wake Fikiri Magoso alisema: “Hapa nyumbani Simba iliwafunga hao Mimosas na wao nyumbani kwao wakafungwa ndio mpira. Kila timu inatumia uwanja wa nyumbani, hivyo mchezo wa mwisho utakuwa kwa Mkapa naamini wachezaji wakikomaa wanapata alama tatu na kutinga hatua inayofuata.”