KAZI ya usajili wa dirisha dogo ni kuzisaidia timu kuboresha upungufu katika vikosi zikisajili mastaa wa kuongeza nguvu.
Zipo timu zinazonufaika na usajili huo – wa dirisha dogo, huku zingine zikiambulia maumivu kuchukua wachezaji wanaoshindwa kuendana na malengo ya timu na kuishia kuonyesha viwango vya chini.
Hiki hapa kikosi cha mastaa 11 waliosajiliwa na timu mbalimbali za Ligi Kuu Bara dirisha dogo msimu huu ambao wameongeza nguvu na kuondoa upungufu vikosini.
ABOUTWALIB MSHERY (YANGA)
Ndiye kipa namba mbili wa Yanga nyuma ya Djigui Diarra, lakini tangu ajiunge na timu hiyo akitokea Mtibwa Sugar, Mshery ameonyesha kiwango bora katika mechi nne alizodaka akiwa hajaruhusu bao ‘cleen sheet’ nne dhidi ya timu za Dodoma Jiji walikoshinda 4-0, wakaifunga Coastal Union 2-0, Polisi Tanzania (1-0) na Mbeya City (suluhu). Mshery ameonyesha ubora na akikosekana Diarra kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi hawezi kupata presha ya kipa wa kulinda matokeo.
DAVID KAMETA ‘DUCHU’ (GEITA GOLD)
Simba ilimpeleka kwa mkopo beki namba mbili, David Kameta ‘Duchu’ katika timu ya Biashara United baadaye akachukuliwa na Geita Gold kupitia usajili wa dirisha dogo, ambapo amekuwa panga pangua ndani ya kikosi hicho.
ADEYUN SALEH (GEITA GOLD)
Alihudumu Yanga kwa miaka miwili, lakini changamoto ya namba kikosini ilifanya asiongezewe mkataba mpya na Wanajangwani, hivyo alikwenda kujiunga na Geita Gold kupitia usajili wa dirisha dogo na amekuwa akiupiga mwingi.
JUMA NYOSO (GEITA GOLD)
Geita Gold iliimarisha safu ya ulinzi kwa kumnasa pia beki mkongwe, Juma Nyoso ikimtoa Ruvu Shooting.
KELVIN YONDANI (GEITA GOLD)
Baada ya kuhudumu kwa msimu mzima akitokea Polisi Tanzania, Kelvin Yondan amekuwa mchezaji tegemeo kwenye kikosi cha kwanza cha Geita Gold.
SALUM ABOUBAKAR ‘SURE BOY’ (YANGA)
Baada ya kiungo mkabaji, Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ kuitumikia Azam FC kuanzia 2007-2021, Yanga ilinasa saini yake na sasa ni msaada ndani ya kikosi hicho.
HARUNA CHANONGO (RUVU SHOOTING)
Chanongo ni ingizo jipya katika kikosi cha kocha Boniface Mkwasa wa Ruvu Shooting na tangu amejiunga kikosini akiwa mchezaji huru baada ya kukaa nyumbani kwa miezi sita, amekuwa ni nyota tegemeo ambaye ameanza kuonyesha makali yake.
IBRAHIM AJIBU (AZAM)
Alianza na kasi kubwa baada ya kutua Azam FC akitokea Simba alikochezea miaka miwili. Baada ya kutua tu aliingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza licha ya kwamba kwa sasa anapitia kipindi kigumu cha pigania namba kikosini.
HAMIS KIIZA ‘DIEGO’ (KAGERA SUGAR)
Nyota huyu wa zamani wa Yanga na Simba tangu ajiunge na Kagera Sugar ‘Wanankurukumbi’ akitokea klabu ya Proline ya nchini kwao Uganda, amehusika katika mabao manne akifunga moja dhidi ya Simba kisha asisti tatu kwa Hassan Mwaterema (mbili) kwenye mchezo wao na Dodoma Jiji, Mbeya City na Mbaraka Yusuph dhidi ya Namungo.
CLATOUS CHAMA (SIMBA)
Usajili wa kiungo mshambuliaji wa Simba, Clatous Chama ulitikisa kwani alihusishwa na Yanga na hilo lilitokana na alama aliyoacha msimu ulioisha akimaliza ligi akiwa na asisti 15 na mabao nane.
Baada ya kurejea kwa mara nyingine Simba, Chama amefunga mabao matatu ya Ligi Kuu na kuwa mchezaji muhimu wa kikosi cha kwanza.
DENIS NKANE (YANGA)
Kipaji alichonacho kiliwavutia mabosi wa Yanga kumsainisha mkataba baada ya kuitumikia Biashara United.
Alianza maisha yake Yanga taratibu kwenye kikosi hicho chenye ushindani mkubwa wa namba ingawa kadri anavyozidi kucheza anaonyesha uwezo mkubwa na kubeba matumaini ya wana Jangwani wanaohitaji ubingwa wa ligi.
WASIKIE MAKOCHA
Akizungumzia maingizo ya Januari yanavyombamba Ligi Kuu, Kocha wa Kagera Sugar, Francis Baraza anasema nyota wengi waliosajiliwa dirisha dogo wamefanya vizuri kutokana na timu husika kuzingatia mahitaji na pia ushindani uliopo unachangia.
“Kwa kikosi hicho ningetumia mfumo wa 4:3:3 kwa sababu walio wengi wanapenda kushambulia na ukiangalia kiuhalisia nyota hao ni tegemeo katika timu wanazozitumikia,” anasema.
Kocha wa zamani wa Tanzania Prisons, Adolf Rishard anasema: “Dirisha dogo maana yake ni kuboresha upungufu uliyopo vikosini na timu nyingi zimefanikiwa kwa hilo.”